• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wachache wajitokeza kupiga kura Thika na Ruiru

Wachache wajitokeza kupiga kura Thika na Ruiru

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa mji wa Thika walijitokeza kupiga kura alfajiri katika uwanja wa Thika Stadium, lakini idadi ilikuwa ya chini mno.

Ikilinganishwa na mwaka wa 2017 wapigakura waliojitokeza Jumanne hawakufurika uwajani.

Hata hivyo katika kituo hicho cha Thika Stadium,  uchaguzi uliendelea kwa amani bila tatizo lolote.

Jambo la kushangaza ni kwamba vijana hawakujitokeza kwa wingi jinsi ilivyotarajiwa kwani watu wazima ndio walioonekana wengi katika kituo hicho.

Katika kituo cha kura cha Kiboko mjini Thika, wapigakura walikuwa wachache ikilinganishwa na hapo awali.

Mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina ambaye ni mwaniaji wa kujitegemea kwa ugavana Kiambu alipiga kura yake mwendo wa saa nane za mchana huku alielezea kusikitishwa kutokana na wapigakura wachache waliofika kituoni.

“Leo ni wazi kuwa wapigakura wamekuwa wachache katika kituo hiki. Vijana wengi pia wanaonekana hawakufika kwa wingi vile ilivyotarajiwa. Muda wa saa tatu zilizosalia kwa sasa ni muhimu kwa wapigakura kuleta mabadiliko,” alifafanua Bw Wainaina.

Mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina ambaye ni mwaniaji wa kujitegemea kwa ugavana Kiambu akipiga kura. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Bw ‘Wajungle’ alisema ana uhakika atachaguliwa kama gavana wa Kiambu.

Aliwarai vijana wasichelewe kupiga kura bali muda mchache uliokuwa umebaki wautumie kufika vituoni kupiga kura.

Bw William Kabogo ambaye alikuwa gavana wa Kiambu hapo awali alipiga kura yake katika kituo cha St George’s kilichoko mjini Ruiru.

Alisema vijana wengi hawakujitokeza kwa wingi jambo ambalo halionyeshi picha nzuri.

“Ninawasihi wale hawajapiga kura wafike kwa wingi ili watekeleze wajibu wao wa kikatiba. Kwa hivyo wapigakura wasichukulie jambo hilo kwa mzaha,” alifafanua Bw Kabogo.

  • Tags

You can share this post!

Korir kutetea taji la New York Marathon mnamo Novemba 6

Mshangao jina la Ngilu kuwa debeni

T L