• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 2:58 PM
Waiguru na Wamatangi watiana kucha bungeni

Waiguru na Wamatangi watiana kucha bungeni

Na PETER MBURU

GAVANA wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru Jumatatu walijibizana na seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi wakati alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu, gavana huyo akishika mori na wakati mmoja kukaidi kujibu maswali ya seneta huyo.

Mgogoro ulianza wakati seneta Wamatangi alidai kuwa Kaunti ya Kirinyaga ilikosa kuwasilisha nakala za kutosha mbele ya kamati ili kuwafanya maseneta kuzipitia na kuuliza maswali, Bi Waiguru akisema huenda yalikuwa makosa madogo na kumtaka seneta huyo kutokuwa na kinyongo katika mazungumzo hayo.

Bi Waiguru aidha alimkosoa seneta huyo kuwa hakuwa akimpa fursa ya kujibu maswali baada ya kuyauliza, akishangaa sababu ya kuyauliza ilikuwa nini.

“Ikiwa siwezi kupewa fursa ya kujibu hata aya ama sentensi kabla ya kuvurugwa, nitakujibu vipi?” Bi Waiguru akauliza wakati fulani.

Mambo yalipochacha, Bw Wamatangi naye alisisitiza kuwa sharti angeuliza maswali ikiwa hajaridhika, akisema “hatuwezi kunyamaza wakati pesa zimepotea ama kuruhusu vijisababu vya wafanyakazi.”

Bi Waiguru wakati fulani alikosa kujibu swali la seneta huyo, akimwachia mmoja kati ya maafisa ambao walikuwa wameandamana mbele ya kamati hiyo kujibu.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa gavana na seneta kujibizana, kwani wakati Gavana wa Isiolo Mohammed Kuti alifika mbele ya kamati hiyo, Seneta wa kaunti hiyo Fatuma Dulo alimshambulia muda wote wa kikao, akiendeleza vita vya kisiasa baina yao, vya kaunti.

You can share this post!

Jaji apinga Rais akiteua jopo la kumchunguza

Naogopa Mungu na uji moto pekee, Waititu aropokwa

adminleo