• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wajackoyah atishia kususia mdahalo

Wajackoyah atishia kususia mdahalo

NA LEONARD ONYANGO

MWANIAJI wa urais wa chama cha Roots George Wajackoyah ametishia kususia mdahalo wa wawaniaji wa urais akidai kubaguliwa.

Profesa Wajackoyah alisema kuwa hatashiriki mdahalo huo utakaofanyika Jumanne ijayo iwapo hatawekwa kwenye kundi moja na wapinzani wake wakuu Naibu wa Rais William Ruto na mgombea wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

Waandaji wa mdahalo huo wamegawa wawaniaji katika makundi mawili – kundi la kwanza linajumuisha wawaniaji wa urais walio na chini ya asilimia 5 katika tafiti za kura za maoni ambazo zimekuwa zikifanywa.

Kundi hilo linajumuisha Prof Wajackoyah na mwenzake David Mwaure Waihiga wa Agano.

Kundi la pili linajumuisha Dkt Ruto na Bw Odinga ambao tafiti zimekuwa zikionyesha kuwa wako bega kwa bega kwa zaidi ya asilimia 30.

Ripoti ya utafiti uliotolewa hivi karibuni na kampuni ya Tifa inaonyesha kuwa Bw Odinga anaongoza kwa asilimia 42 huku Dkt Ruto kwa asilimia 39 na Prof Wajackoyah na Bw Waihiga wako na chini ya asilimia 5.

Ripoti ya hivi karibuni ya Infotrak ilionyesha kuwa Bw Odinga anaongoza kwa asilimia 49, Dkt Ruto (asilimia 30) na Prof Wajackoyah (asilimia 5).

“Nchini Amerika, Uingereza na Canada wawaniaji wote wanafika kwa wakati mmoja kuulizwa maswali. Mimi sio samaki mdogo, ni samaki mkubwa sawa na Ruto na Raila.

“Mbona Kenya wawaniaji wa urais wanabaguliwa kwa misingi ya ripoti ya kura ya maoni iliyofanywa na kampuni ambazo haziaminiki?” akauliza Prof Wajackoyah.

Alihoji ripoti hizo akisema kuwa zinapotosha kuhusu umaarufu wa Naibu wa Rais Ruto na Bw Odinga.

“Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa kuna pengo kubwa kati ya Bw Odinga na Naibu wa Rais. Lakini ukweli ni kwamba pengo ni finyu sana kwani kuna ushindani mkali baina yao.

“Ukweli ni kwamba ikiwa Raila ameshinda Ruto anafaa kumzidi kwa asilimia zisizozidi mbili,” akasema Prof Wajackoyah.

Msomi huyo wa sheria alisema kuwa waandaaji wa mdahalo wa urais hawajawahi kutuuliza sisi wawaniaji kuhusu ni kampuni ipi tunaamini kufanya utafiti wa kura ya maoni.

Mwaniaji huyo wa urais ambaye amezua mjadala mkali nchini kutokana na ahadi yake ya kutaka kuhalalisha bangi iwapo atachaguliwa, alidai kuwa ana umaarufu mkubwa katika Kaunti za Nairobi na Meru ikilinganishwa na Bw Odinga na Naibu wa Urais.

“Inasikitisha kuwa kampuni za kura ya maoni zinanipa asilimia moja jijini Nairobi na Meru ilhali mimi ndiye ninaongoza. Nitashinda urais hata bila kuhudhuria mdahalo,” akasema Prof Wajackoyah.

Alidai kuwa Bw Odinga na Naibu wa Rais Ruto wametuma majasusi kufuatilia mienendo yake.

Mdahalo wa marais utafanyika Julai 26 katika Chuo Kikuu cha Catholic Eastern Africa (CUEA) mtaani Karen, Nairobi.

Wakenya walio na maswali wanahitaji kuyatuma mapema kupitia nambari ya arafa: 22843 au kwa njia ya video: nambari ya WhatsApp: 0796560560.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru ateua majaji saba wapya katika mahakama ya rufaa

Mwaniaji alenga kura kwa ahadi ya pombe

T L