• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Mwaniaji alenga kura kwa ahadi ya pombe

Mwaniaji alenga kura kwa ahadi ya pombe

NA ALEX KALAMA

MGOMBEAJI ugavana katika Kaunti ya Kilifi kupitia Chama cha PAA, George Kithi, ameahidi kununulia wapigakura pombe ya mnazi baada ya Uchaguzi Mkuu ili waepuke kulewa mkesha wa Agosti 9.

Katika hali inayoonekana kuwa ya kuepusha kura zozote kupotea kwa sababu ya ulevi, Bw Kithi alisema atatimiza ahadi hiyo kama tu wapigakura watachagua viongozi wa PAA.

“Ikifika tarehe nane ya mwezi wa nane, ule mnazi wote unaokuja hapa tutaufunga na tutalipa na hakuna mtu atauziwa mnazi. Watu wataenda kupiga kura, tukishinda, ule mnazi wote watu wanywe,” alisema Bw Kithi, akizungumza na wakazi wa Mtwapa, eneobunge la Kilifi Kusini.

Wanasiasa katika pembe tofauti za nchi wamekuwa wakitoa mapendekezo ya ajabu yanayolenga kuhakikisha kila mpigakura anafika kituoni siku ya uchaguzi.

Baadhi ya mapendekezo mengine ambayo yamegonga vichwa vya habari ni kama vile, wake kuambiwa wanyime waume zao huba hadi wahakikishe wamepiga kura.

Kwingineko, aliyekuwa mbunge wa Malindi, Bw Lucas Maitha, amelitaka bunge la kaunti ya Kilifi kuunda sheria itakayowezesha pombe ya mnazi kuwa katika soko la kitaifa na kimataifa.

“Kwa sababu kilimo kimegatuliwa na huu mnazi unahusiana na kilimo, lazima bunge la kaunti (lijalo) lipitishe mswada ili mnazi upate soko la kisawasawa ndani ya taifa la Kenya na hata mataifa ya nje. Na waanze kusaidia hawa watu wa mnazi kwa kutafuta masoko nje ya Kilifi,” alisema Bw Maitha.

  • Tags

You can share this post!

Wajackoyah atishia kususia mdahalo

Kalonzo atikisa Azimio na wito wa suti ya Wiper Kitui

T L