• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Walioanguka mchujo UDA kutozwa hadi Sh200,000

Walioanguka mchujo UDA kutozwa hadi Sh200,000

NA MARY WANGARI

WAGOMBEAJI wa United Democratic Alliance (UDA) wanaopinga matokeo ya kura za mchujo zilizofanyika Alhamisi, sasa watalazimika kulipa kati ya Sh20,000 na Sh200,000 ili kuwasilisha malalamishi yao kwa chama.

Hii ni baada ya usimamizi wa chama hicho, kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kutangaza ada za malipo kwa wawaniaji wote wanaotaka kuwasilisha malalamishi kuhusu michujo hiyo.

Kulingana na taarifa iliyofikia Taifa Leo jana kutoka kwa Kamati ya UDA ya Kutatua Malalamishi kuhusu Chaguzi na Teuzi za Mchujo (EDRC), wawaniaji hao watalipia ada mbalimbali kwa viti walivyokuwa wakisaka.

Wawaniaji wa udiwani watatozwa Sh20,000, kiti cha ubunge na useneta Sh100,000 kila moja huku kile cha ugavana kikitozwa Sh200,000.

“Malipo kuhusu ada inayohitajika ili kuwasilisha malalamishi yanafafanuliwa katika Kitengo C cha Sheria.

Ni kama ifuatavyo: uchaguzi wa urais Sh500,000, ugavana Sh200,000, useneta Sh100,000, bunge Sh100,000, Mbunge Mwakilishi wa Kike Sh100,000 na udiwani Sh20,000,” ilieleza taarifa hiyo.

Ikaongeza: “Malipo yote yanapaswa kutumwa kupitia tu njia ya Mpesa nambari ya Pay- Bill 888092, jina la akaunti na nambari ya kitambulisho ya mlalamishi. Kamati ya EDRC itaandaa vikao kusikiza malalamishi katika jumba la Hustler Center.” Hatua hii imejiri baada ya idadi kubwa ya wawaniaji ambao hawakuridhishwa na matokeo ya kura za mchujo zilizoandaliwa Alhamisi, kufurika katika makao makuu ya UDA wakishinikiza mchakato huo ulikumbwa na ghasiana hivyo ufutiliwe mbali.

Tangazo hilo limeonekana kuibua hisia kali miongoni mwa wafuasi wa UDA huku wengi wakinyooshea kidole cha lawama usimamizi wa chama kwa matokeo hayo duni ya mchujo.

“Diwani alipe Sh20,000 ilhali ni makosa yenu; mnajali tu pesa.

“Kwa mfano, katika kituo changu cha kupigia kura hakuna vifaa vya kura vililetwa ilhali wadi yote ilipiga kura,” alifoka Leonard Ronoh.

“Ni wazi kabisa chama hakina nia ya kusikiza malalamishi. Mbona mwaniaji aliyelipa Sh500,000 kama ada ya kushiriki mchujo alipe tena Sh200,000 ili malalamishi yake yasikizwe? ” alihoji Dan Mahiri.

“Katika eneobunge la Roysambu zoezi la upigaji kura halikuambatana na sheria, hasa kwenye Wadi ya Zimmerman ambapo makarani na wasimamizi wa vituo hawakuwepo. Isitoshe uchaguzi ulianza saa tisa jioni,” akaeleza Joseph Kamau.

Huku wawaniaji na wafuasi wakilalamikia vikali changamoto zilizokumba mchujo wa UDA, Dkt Ruto, anayegombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwezi Agosti, alisisitiza shughuli ilifanyika kwa njia ya amani.

“Upigaji kura katika kaunti 36 ulifanyika kwa njia shwari baada ya matatizo madogodogo na changamoto za kiutendakazi kutatuliwa,” akatanguliza kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Pongezi kwa wawaniaji wetu wote 5,000 kwa kuwa na subira na utulivu. Viti 888 viligombewa huku maafisa 49,811 wa uchaguzi wakishirikishwa katika vituo 16,513,” aliongeza Naibu Rais.

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaongeza muda wa kusajili laini za simu hadi...

Brighton yazamisha Spurs

T L