• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
Wanaodandia vinara wakuu

Wanaodandia vinara wakuu

Na LEONARD ONYANGO

HOFU ya kuangushwa kwenye mchujo na wawaniaji chipukizi imesukuma baadhi ya wanasiasa kung’ang’ania wakuu wa vyama vyao ili wapewe tiketi za moja kwa moja kuwania viti katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wanasiasa hao wamegeuka watetezi sugu na wamekuwa wakiandamana na vinara wa vyama vyao katika mikutano mbalimbali na kuwamiminia sifa tele katika juhudi za kusaka tiketi.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa, baadhi ya wabunge wamekuwa wakianzisha miradi kwa kutumia fedha za Hazina ya Ustawishaji Maeneobunge (CDF-NG) na kisha kualika vigogo wa vyama vyao kuizindua ili kushtua wapinzani wao.

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri alimwalika Naibu wa Rais William Ruto wikendi iliyopita kufungua rasmi Kituo cha Polisi cha Lanet, Kaunti ya Nakuru, katika kile kimefasiriwa kuwa juhudi za kunyamazisha wapinzani wake.

“Usalama ni muhimu katika ukuaji wa biashara za ‘mahasla’ (walalahoi). Ninashukuru sana Bw Ngunjiri kwa kuwekeza katika usalama,” alisema Dkt Ruto wakati wa ufunguzi huo.

Wadadisi wa siasa wanasema Bw Ngunjiri alimwalika Dkt Ruto kupunguza upinzani mkali unaomkabili kutoka kwa Bi Irine Njoki ambaye ni msaidizi wa Waziri wa Uchukuzi, James Macharia.

Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi huenda pia akanusuriwa na ukaribu wake na Naibu wa Rais Dkt Ruto kuhifadhi kiti chake.

Bw Sudi anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Bw Francis Murgor, mtaalamu wa masuala ya fedha na teknolojia ambaye amejizolea uungwaji mkono miongoni mwa vijana, Bi Pauline Tuwei, mbunge wa zamani David Koros na mfanyabiashara Steve Kewa.

Mbunge wa Soy Caleb Kositany sasa anamezea mate ugavana wa Uasin Gishu huku akitarajia kuwa, ukaribu wake na Dkt Ruto utamsaidia kupata tiketi ya moja kwa moja. Bw Kositany anamenyana na Naibu Gavana Daniel Chemno ambaye ni mwandani wa Bw Sudi.

Katika Kaunti ya Nandi, Seneta Samson Cherargei ambaye ni mtetezi mkuu wa Dkt Ruto, ametangaza azma ya kumng’oa Gavana Stephen Sang katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wengine ambao wanatarajia kupewa tiketi ya UDA ya moja kwa moja kutokana na ukaribu wao na Dkt Ruto ni Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na wabunge Ndidi Nyoro (Kiharu), Aisha Jumwa (Malindi), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Mohammed Ali (Nyali), Rigathi Gachagua (Mathira) na Magavana Anne Waiguru (Kirinyaga) na Mutahi Kahiga (Nyeri) kati ya wengineo.

Jumapili, Dkt Ruto alishikilia kuwa chama cha UDA kitaandaa kura za mchujo kwa njia huru na haki.

“Usije kusimama na mimi tupigwe picha halafu uanze kuzisambaza ukidai kwamba umepewa tiketi ya moja kwa moja. Kura za mchujo zitakuwa huru na haki kwa kila mmoja,” akasema Dkt Ruto alipokutana na wanasiasa wanaomezea viti mbalimbali kupitia tiketi ya UDA jijini Nairobi.

Kiongozi wa ODM Bw Odinga anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa naibu wake Wycliffe Oparanya za kutaka baadhi ya wanasiasa wa chama hicho wapewe tiketi za moja kwa moja.

“Tunataka kubadili mfumo ili tusifanye kura za mchujo na badala yake tutoe tiketi za moja kwa moja au wawaniaji wateuliwe na wajumbe wachache wa chama,” anasema Bw Oparanya.

Bw Odinga tayari ametangaza kuwa watakaoshiriki kuteua wawaniaji wa ODM ni sharti wawe na kadi ya uanachama tofauti na awali ambapo mtu yeyote alishiriki kwa kupiga kura katika mchujo.

Bw Martin Andati, mdadisi wa masuala ya siasa anaonya kuwa, kutoa tiketi moja kwa moja kutakuwa pigo kwa chama cha ODM kwani watakaonyimwa tiketi huenda wakahamia kambi ya Dkt Ruto.

Mfanyabiashara Bruno Liende na mtaalamu wa masuala ya mazingira Samuel Amimo ambao wametangaza azma ya kuwania ubunge wa Suna Mashariki, sasa wanahofia kuwa mshindani wao mkubwa mbunge wa sasa Junet Mohamed, huenda akapewa tiketi ya moja kwa moja kutokana na ukaribu wake na Bw Odinga.

“Tunachohitaji ni usawa na haki katika kura za mchujo. Hatutakubali mtu kupendelewa na chama,” Bw Amimo akaambia Taifa Leo.

Miongoni mwa wanasiasa wa ODM ambao wanaamini ukaribu wao na Bw Odinga utawapa tiketi ya moja ni wabunge Mishi Mboko (Likoni), John Mbadi (Suba Kusini), Babu Owino (Embakasi Mashariki) na Gavana Anyang Nyong’o (Kisumu) na mfanyabiashara Suleiman Shahbal.

Bw Shahbal ambaye anamezea mate ugavana Kaunti ya Mombasa, amekuwa akiandamana na Bw Odinga katika hafla mbalimbali kote nchini. Gavana wa Mombasa Hassan Joho, hata hivyo, Jumapili alitangaza kuwa ataunga mkono mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir kuwa mrithi wake – hivyo kumweka Bw Odinga katika njiapanda.

Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala na mbunge wa Lugari Ayub Savula wamekuwa wakishindana kuonyesha utiifu wao kwa kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ili kupata tiketi ya moja kwa moja. Bw Malala na Bw Savula wote wanamezea mate kiti cha ugavana wa Kakamega.

Gavana wa Kitui Charity Ngilu, wiki iliyopita, alimuonya kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, kujihadhari na marafiki feki ambao wanataka kutumia ‘jina’ lake kushinda viti katika uchaguzi ujao.

“Wanasiasa wanaokuzunguka wanakuimbia nyimbo za sifa na kukudanganya kwamba utakuwa rais wa tano. Lakini ukweli ni kwamba, wanakudanganya na lengo lao ni kushinda viti,” akasema Bi Ngilu.

Baadhi ya wanasiasa ambao wamejitokeza kuwa wapiganiaji wa Bw Musyoka ni Seneta wa Kitui Wambua Enoch na Balozi wa Kenya nchini Uganda Kiema Kilonzo ambaye anamezea mate ugavana wa Kitui mwaka ujao.

Maelezo ya ziada na ERIC MATARA

You can share this post!

TAHARIRI: Wanasiasa wakome kutoa ahadi ambazo haziwezi...

Mwanamke abakwa na kutupwa kwa maji machafu Mukuru

T L