• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Wanaopiga jeki Raila katika safari ya ikulu

Wanaopiga jeki Raila katika safari ya ikulu

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

MKONO FICHE WA serikali unaonekana kuendesha kampeni za kiongozi wa ODM Raila Odinga. Ingawa Bw Odinga ameshikilia kwamba yeye si mradi wa serikali, kampeni zake zimekuwa zikipigwa jeki na maafisa wa serikali pamoja na washirika wa Rais Uhuru Kenyatta.

Tofauti na Naibu wa Rais William Ruto ambaye amekuwa akitumia wabunge na madiwani kupenya katika maeneo mbalimbali ya nchi kusaka kura, Bw Odinga anatumia magavana, mawaziri na maafisa wengine wa serikali.

Dkt Ruto anaungwa mkono na magavana wawili pekee nje ya ngome yake – eneo la Bonde la Ufa – ambao ni Bw Okoth Obado (Migori) na Bi Anne Waiguru (Kirinyaga) ambaye alitangaza kugura Jubilee na kujiunga na cha chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto.

Bw Odinga anaungwa mkono na zaidi ya nusu ya magavana wa kaunti 47 nchini na baadhi yao wakiwa wandani wa Rais Uhuru Kenyatta.Katika eneo la Mlima Kenya ambalo ni ngome ya Rais Kenyatta, kwa mfano, Bw Odinga anaungwa mkono na Magavana Ndiritu Muriithi (Laikipia), James Nyoro (Kiambu), Mutahi Kahiga (Nyeri), Lee Kinyanjui (Nakuru), Kiraitu Murungi (Meru), Martin Wambora (Embu) na Muthomi Njuki (Tharaka Nithi).

Magavana hao ni washirika wakuu wa Rais Kenyatta.Katika eneo la Ukambani, Bw Odinga anaungwa mkono na magavana wote watatu; Bi Charity Ngilu (Kitui), Prof Kivutha Kibwana (Makueni) na dkt Alfred Mutua (Machakos).Jana, wandani wa Dkt Ruto walidai Rais Kenyatta amelazimisha magavana hao kuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais wa Agosti 9, 2022.

Wandani wa Naibu wa Rais waliokuwa wakizungumza kwenye msururu wa mikutano ya kisiasa katika Kaunti ya Kitui, walidai magavana wanaounga mkono wametishiwa kushtakiwa endapo wataunga mkono Dkt Ruto.

“Magavana wanaunga Raila Odinga kwa sababu wameambiwa kuwa wakiunga Dkt Ruto watashtakiwa,” akadai Bw Nimrod Mbai, mbunge wa Kitui Mashariki.Dkt Ruto pia amekuwa akitoa madai sawa na hayo katika mikutano yake ya kisiasa.

Inaonekana madai hayo ya Dkt Ruto yanatokana na hofu kwamba, ushawishi wa magavana hao katika kaunti zao huenda ukasaidia pakubwa kumzolea kura nyingi Bw Odinga katika Uchaguzi Mkuu ujao.Mawaziri Sicily Kariuki (Maji), Joe Mucheru (Teknolojia na Mawasiliano- ICT), Fred Matiang’i (Usalama), Peter Munya (Kilimo), John Munyes (Madini), Eugine Wamalwa (Ulinzi) na Margaret Kobia (Huduma kwa Umma) ni miongoni mawaziri ambao wametangaza wazi kumuunga mkono Bw Odinga.

Hata hivyo, Bw Odinga, Alhamisi, alipuuzilia mbali madai kwamba yeye ni ‘mradi’wa Rais Kenyatta.“Haiwezekani mimi kuwa mradi wa mtu. Nikisikia madai hayo huwa ninacheka sana. Hata Rais Kenyatta anacheka akisikia kwamba mimi ni mradi wake.

Mimi ni mradi wa Wakenya,” akasema.Mabwanyenye wa wakfu wa Mount Kenya Foundation (MKF) – waliosaidia Rais Kenyatta kushinda uchaguzi mara mbili – pia wamekuwa wakimsaidia Bw Odinga kuendesha kampeni zake.

Bwanyenye Samuel Kamau Macharia, maarufu kama SK, mwanachama wa MKF, amekuwa akitumia rasilimali zake kupigia debe Bw Odinga.Wikendi iliyopita, Bw Macharia alikuwa miongoni mwa watu maarufu walioandamana na Bw Odinga kwenye ziara ya kuvumisha nia yake ya urais katika Kaunti ya Nyandarua.

Taifa Leo imebaini kuwa mabwanyenye wa MKF ndio wametwikwa jukumu na Rais Uhuru Kenyatta kufanya majadiliano na vyama vidogo ili kuvishawishi kuunga mkono Bw Odinga. Mabwanyenye wa MKF pia wanaendelea na juhudi za kushawishi vigogo wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kuunga mkono kinara wa ODM.

Bw Odinga, Alhamisi, alikiri kuwa mazungumzo baina yake na viongozi wa OKA yanaendelea.

You can share this post!

Boda waonywa dhidi ya kuhusika katika ghasia 2022

Watawanywa kwa vitoa machozi huku wakidai haki

T L