• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Wanasiasa wabuni njama IEBC ikisajili wapigakura wapya

Wanasiasa wabuni njama IEBC ikisajili wapigakura wapya

IDADI ndogo ya wananchi walijitokeza Jumatatu katika kaunti za Pwani kwa usajili wa wapigakura wapya, huku baadhi ya viongozi wakidaiwa kutumia mbinu chafu ili waongeze idadi katika maeneobunge yao.

Katika Kaunti ya Kisii, Mbunge wa Mugirango Kusini, Bw Sylvanus Osoro, alitishia kuwanyima basari watoto ambao wazazi wao hawatakuwa wamejisajili kupiga kura kufikia wakati shule zitakapofunguliwa muhula ujao.

Bw Osoro ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, alisema wale watakaojiandikisha kutaka basari watahitajika kuambatisha thibitisho la kuonyesha wazazi wao walijisajili kupiga kura katika ombi lao.

“Hata kama unampenda William Ruto, bila kadi ya kura hutamsaidia. Mugirango Kusini baada ya mwezi mmoja tutatangaza basari. Kama huna kadi ya kura hutapata basari. Badala ya kitambulisho tunataka kadi ya kupiga kura,” akatishia.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inalenga kusajili wapigakura wapya milioni sita kitaifa, wengi wao wakiwa ni vijana ambao hawakuwa wamefikisha umri wa miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Mbunge wa Ganze, Kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire kwa upande wake alidai kuwa baadhi ya wanasiasa walikuwa wakiendeleza njama ya kuwasafirisha wapigakura kutoka maeneo ya nje ili wajiongeze ufuasi kabla uchaguzi ujao.

Bw Mwambire aliambia Taifa Leo kuwa aliarifiwa Jumapili kuhusu mipango hiyo anayodai inaendelezwa na wapinzani wake.

“Niko na watu pembe zote ambao wanafuatilia shughuli hii ili kuhakikisha inafanikishwa ipasavyo. Niliambiwa kuwa kuna magari 10 ambayo yalikodishwa kuwachukua watu kutoka sehemu za Mtwapa, Kilifi, Tezo na sehemu nyingine,” akasema.

Bw Mwambire alisema wanasiasa katika eneobunge hilo wanaogombea kiti cha ubunge wamekuwa na desturi hiyo ambayo huwaacha wakihangaika baadaye.

Katika Kaunti ya Mombasa, vituo vingi vya kusajili wapigakura havikuwa vimepokea watu kufikia Jumatatu mchana.

Kituo kilicho katika uwanja wa Makadara, eneobunge la Mvita kilikuwa kimetembelewa na watu wawili pekee kufikia wakati huo, huku afisi ya IEBC ikipokea mmoja pekee.

Wakazi wengi waliohojiwa na Taifa Leo walisema hawakujua kama usajili ulikuwa unaendelea.

“Nilikuwa nimekuja hapa kwa shughuli zangu ndipo nikafahamu kumbe usajili unaendelea. Lakini nitajisajili siku nyingine, si leo,” Bw Omar Salim, alisema akiwa Makadara.

Mratibu wa uchaguzi katika eneobunge la Mvita, Bi Neema Karisa, alisema watazunguka katika wadi zote ili kufikisha lengo lao la kusajili wapigakura wapya 24,651.

Akizindua shughuli ya usajili katika Kaunti ya Nakuru, Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, alisema usajili utafanywa kila siku ikiwemo wikendi kwa siku 30.

“Tunawaomba Wakenya hasa vijana wajitokeze kwa wingi kujisajili,” akasema Bw Chebukati.

Ripoti za Maureen Ongala, Eric Matara, Valentine Obara na Wachira Mwangi

You can share this post!

TAHARIRI: Vijana wapewe vitambulisho upesi

Wafugaji watishia kususia misaada wasipopewa pia lishe ya...