• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Wanjigi avamia Mlimani kusaka kura za urais

Wanjigi avamia Mlimani kusaka kura za urais

Na NICHOLAS KOMU

MFANYABIASHARA Jimi Wanjigi, ambaye ametangaza azma ya kuwania urais mwaka 2022 ameanzisha kampeni kali ya kusaka uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya; eneo ambalo limegawanyika kisiasa.

Hatua ya Bw Wanjigi inajiri wakati ambapo wagombeaji urais wanang’ang’ania kura za ngome hiyo ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye atastaafu baada ya kukamilisha muhula wake wa pili afisini.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA), kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, na muungano mpya wa One Kenya Alliance (OKA) tayari wameanza kusaka uungwaji mkono kutoka eneo hilo lenye karibu kura milioni tano.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga pia anajizatiti kusaka uungwaji mkono kutoka eneo hilo, kwa kutumia ukuruba kati yake na Rais Uhuru Kenyatta kupitia handisheki.

Bw Wanjigi ambaye pia ametangaza atawania urais kwa tiketi ya ODM ameahidi kushindana na vigogo wengine, akiwemo Bw Odinga, katika mchujo wa kusaka idhini ya kupeperusha bendera ya chama hicho cha chungwa.

Hata hivyo, ODM haina ushawishi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya na hivyo Mbw Wanjigi na Odinga watahitajika kukivumisha kwanza

Hata hivyo, Bw Wanjigi ameelezea matumaini ya kupata uungwaji mkono kutoka eneo la Mlima Kenya kwa msingi kuwa hamna mgombeaji urais mwenye ushawishi mkubwa kutoka eneo hilo.

Hii ni licha ya kwamba Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi pia ametangaza kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais 2022, japo hajatangaza chama atakachotumia.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Bw Wanjigi amekuwa wakifanya mikutano ya faragha na maafisa wa ODM na wapinga mikakati wa kisiasa katika kaunti ya Nyeri.

Hata hivyo, kabla ya kushawishi eneo la Mlima Kenya kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa 2022, anakabiliwa na kibarua cha kupata tiketi ya kupeperusha bendera ya urais katika mchujo.

You can share this post!

Kalonzo azindua sekretarieti ya kushirikisha kampeni zake...

Gloria: Bado malipo ni duni kwenye sanaa ya uigizaji