• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Washirika wa Ruto wamkosoa vikali rais

Washirika wa Ruto wamkosoa vikali rais

Na WANDERI KAMAU

WASHIRIKA wa Naibu Rais William Ruto wamemkosoa vikali Rais Uhuru Kenyatta kufuatia matamshi aliyotoa katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Nyeri, Jumatano, ambapo alimtaja kuwa kiongozi mfisadi na asiye na subira.

Hapo jana Alhamisi, washirika hao walimtaja Rais Kenyatta kuwa mdanganyifu, kwani alificha maovu yanayohusishwa na baadhi ya waandani wake wa karibu.

Mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) alisema ni kinaya kwa Rais Kenyatta kumtaja Dkt Ruto kuwa mfisadi ilhali hajashtakiwa katika mahakama yoyote kufuatia tuhuma hizo.

“Tuhuma hizi dhidi ya Dkt Ruto zimekuwa zikitolewa tangu 2018. Amehusishwa na kila sakata ya ufisadi. Swali langu ni kwa nini hajawahi kushtakiwa katika mahakama yoyote na kupatikana na hatia,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge huyo alisema ili Wakenya kumwamini Rais Kenyatta, lazima aeleze nchi ukweli kuhusu hatua zilizochukuliwa kwa watu waliotajwa kuhusika kwenye sakata ya uporaji wa pesa za kukabiliana na janga la virusi vya corona katika Mamlaka ya Kusambaza Dawa Kenya (KEMSA).

Inakisiwa kuwa zaidi ya Sh7.3 bilioni zilitoweka katika hali tatanishi katika mamlaka hiyo.

“Rais aliipa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) siku 21 kuchunguza na kutoa ripoti kuhusu waliohusika katika sakata hiyo. Mbona watu hao hawajatajwa hadharani kufikia sasa? Mbona Rais anaonekana kurejelea vita dhidi ya ufisadi kwa njia ya ubaguzi?” akashangaa mbunge huyo.

Mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) alisema rais alikataa kutaja baadhi ya sakata kwani kando na washirika wake, yeye mwenyewe na baadhi ya jamaa wake wanahusika.

“Kando na sekta ya KEMSA, Rais Kenyatta aliahidi kutoa taarifa baada ya familia yake kutajwa kwenye sakata ya Pandora Papers, ambapo watu maarufu duniani wameficha mabilioni ya fedha katika nchi za kigeni. Mbona hajafanya hivyo hadi leo?” akashangaa.

Alisema ni kinaya kwa Rais Kenyatta kumtaja Dkt Ruto kama mnafiki, ilhali yeye amekuwa akikwepa kuwaeleza Wakenya ukweli hasa kuhusu sakata zinazowahusisha washirika wake wa karibu.

You can share this post!

Ukraine yaililia dunia Urusi ikiivamia

Wanafunzi 2 kufanya KCSE wakiwa kizuizini

T L