• Nairobi
  • Last Updated June 14th, 2024 4:55 PM
Ukraine yaililia dunia Urusi ikiivamia

Ukraine yaililia dunia Urusi ikiivamia

MASHIRIKA na WANDERI KAMAU

UKRAINE jana Alhamisi iliirai dunia kuungana nayo dhidi ya uvamizi wa Urusi, baada ya majeshi ya Urusi kutekeleza mashambulio kadhaa nchini humo.

Ukraine iliomba msaada wa kijeshi, ikisema uvamizi wa Urusi unahatarisha uhuru na usalama wake.

Uvamizi huo unajiri baada ya Urusi kutangaza kwamba inatambua uhuru wa maeneo mawili yaliyojitenga na Ukraine na ingetuma majeshi yake.

Jana Alhamisi, viongozi mbalimbali duniani waliungana kuikemea Urusi, ikizingatiwa ilikuwa imesema itaheshimu mazungumzo ya kusuluhisha mzozo wake na Ukraine.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, alimkosoa vikali Rais Vladimir Putin kutokana na uvamizi huo.

“Rais Putin, wazuie wanajeshi wako dhidi ya kuishambulia Ukraine. Heshimu nafasi ya mazungumzo. Watu wengi sana tayari washafariki,” akasema kupitia mtandao wa Twitter.

Akaongeza: “Ili kulinda na kuheshimu ubinadamu, warejeshe wanajeshi wako Urusi. Ni lazima vita hivyo viishe sasa.”

Kwenye taarifa, Rais Joe Biden wa Amerika pia alikemea kitendo cha Urusi.

“Rais Putin amechagua njia ya vita ambayo italeta hasara na umwagikaji mkubwa wa damu. Urusi ndiyo itawajibikia vifo na uharibifu utakaosababishwa na uvamizi huo. Hata hivyo, Amerika na washirika wake zitaungana kuikabili kikamilifu,” akasema Biden.

Biden alisema alipokea simu ya dharura kutoka kwa Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, akimwomba kuwarai viongozi mbalimbali duniani “kujitokeza na kukemea ukatili wa Rais Putin na kusimama pamoja na raia wa Ukraine.”

Nchini Uingereza, Waziri Mkuu Boris Johnson alisema nchi yake inaungana na washirika wake “kujibu vilivyo mashambulio ya Urusi.”

Hapo Alhamisi, Baraza la Muungano wa Ulaya liliitisha kikao cha dharura, ambacho kilitarajiwa kujadiliana kuhusu vikwazo watakavyoiwekea Urusi.

Mkuu wa baraza hilo, Charles Michel na mwenzake wa Tume ya Muungano wa Ulaya (EUC), Ursula von de Leyen, walisema kwa pamoja kuwa “uvamizi huo hauna nafasi katika karne ya 21.”

“Tunairai Urusi kukomesha ukatili wake dhidi ya Ukraine kwa kuondoa majeshi yake kutoka taifa hilo. Inapaswa kuheshimu uhuru na mipaka ya Ukraine,” wakaeleza.

Jumanne, Muungano wa Ulaya (EU) ulitangaza vikwazo kadhaa ambavyo vinalenga benki zinazodaiwa kufadhili shughuli za kijeshi za Urusi na zile zinaunga mkono hatua ya Urusi kutambua uhuru wa maeneo hayo mawili yaliyojitenga na Ukraine.

Balozi wa Ukraine nchini Kenya, Andzii Pzavednyk, alisema dunia inapaswa kuiwekea Urusi vikwazo vikali kwa kutoheshimu mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kusuluhisha mzozo huo.

Mvutano huo ulianza mnamo 2014, baada ya Urusi kuivamia Ukraine na kuchukua udhibiti wa eneo tata la Crimea.

Licha ya rai kutoka kwa viongozi mbalimbali duniani, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), Urusi inashikilia kwamba lazima “itetee maeneo yake.”

  • Tags

You can share this post!

Mwandishi ‘adui’ wa Museveni atoroka UG

Washirika wa Ruto wamkosoa vikali rais

T L