• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Washirika wa Ruto wazidi kuponda Uhuru

Washirika wa Ruto wazidi kuponda Uhuru

NA GEORGE MUNENE

VIONGOZI wa muungano wa Kenya Kwanza, Jumamosi waliendeleza shutuma zao kwa Rais Uhuru Kenyatta wakimsuta kwa kumsaliti naibu wake Dkt William Ruto.

Wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, viongozi hao walisisitiza kuwa Dkt Ruto alimuunga mkono Rais Kenyatta katika chaguzi za 2013 na 2017.

Licha ya hayo walielezea kusikitishwa kwao na hatua ya kiongozi wa taifa kumtelekeza naibu wake na kuamua kumuunga mkono mgombea urais wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga.

Wakihutubia mikutano ya kampeni katika masoko ya Gatuiri na Baricho, kaunti ya Kirinyaga, wanasiasa hao walimtaja Rais Kenyatta kama mtu asiye na shukrani.

“Rais alishinda uchaguzini mara mbili kwa sababu ya Ruto lakini sasa anamuunga mkono Odinga kuwa mrithi wake. Juhudi hizo zitaambulia patupu,” akasema Profesa Kindiki.

Akaendelea: “Kenyatta vile vile alikataa kushiriki katika marudio ya uchaguzi wa urais baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017. Lakini Ruto alimshauri asivunjike moyo na alipokubali kushiriki aliibuka mshindi.”

Wanasiasa hao pia walidai kuwa Rais Kenyatta aliwasaliti wakazi wa Mlima Kenya alipofaulu 2017 lakini baadaye akafanya mazungumzo na Bw Odinga.

“Baada ya kumsaidia kupata mamlaka, Rais alitupokonya nyadhifa za uongozi katika kamati za bunge na akatufurusha kutoka serikalini. Sasa Rais anatulazimishia Odinga. Hii sio haki. Atuache tuendelee na harakati za kujiandalia mustakabali wetu kisiasa,” akaongeza Profesa Kindiki.

Wanasiasa hao walimtaka Rais astaafu kwa amani na atoe nafasi kwa Wakenya kumchagua kiongozi wanayemtaka kuwa mrithi wake.

“Inaudhi kwamba Rais Kenyatta hata amewashauri Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na Katibu wake Karanja Kibicho kumfanyia kampeni Odinga. Hatutakubali hilo. Rais na Odinga watafunganya virago vyao na kuenda nyumbani pamoja Agosti 9,” akasema Bw Muturi.

Viongozi hao pia walimpigia debe Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na kumtaja kama anayefaa kuchaguliwa tena.

“Waiguru ameanzisha miradi mingi ya maendeleo katika kaunti hii na anafaa kuchaguliwa tena ili aendelee kuimarisha maisha ya wakazi,” akasema Bw Muturi, ambaye ni kiongozi wa chama cha Democratic Party (DP).

Gavana Waiguru naye alikuwa na la kusema.

“Tunataka Ruto achaguliwe kwa kura nyingi kwa sababu ni kiongozi mchapakazi. Tunawaomba muelekeze kura zenu zote kwa debe la Dkt Ruto,” Bi Waiguru akasema.

Bw Muturi alisema kuwa ni Dkt Ruto anayeelewa shida za raia wa kawaida na anafaa kuchaguliwa kuwa rais wa tano.

“Kupitia mfumo wa kuchochea ukuaji wa uchumi kuanzia ngazi za mashinani (Bottom Up), Ruto ataimarisha maisha ya Wakenya na ndiye anafaa kumrithi Rais Kenyatta,” akasema Bw Muturi.

Spika huyo alisema manifesto ya Dkt Ruto iliyozinduliwa Juni 30 ndiyo bora zaidi kwani ameahidi kuimarisha biashara za raia wadogo kwa kuwapa mikopo yenye riba ya chini.

  • Tags

You can share this post!

Ombi Waislamu wadumishe amani uchaguzi ukinukia

TAHARIRI: Kila mtu ajikinge msimu huu wa baridi

T L