• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
TAHARIRI: Kila mtu ajikinge msimu huu wa baridi

TAHARIRI: Kila mtu ajikinge msimu huu wa baridi

NA MHARIRI

MSIMU wa baridi kali uko nasi na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa inasema utaendelea kwa muda.

Huu ni msimu ambao unaandamana na hatari nyingi yakiwemo maradhi kama vile kichomi, mafua na homa kali.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa walio hatarini zaidi ni watoto na wazee ambao kinga ya miili yao iko chini.

Hivyo basi, kila mmoja anafaa kuhakikisha kwamba amekinga watoto na wazazi walio na umri mkubwa dhidi ya baridi kali ili kuepuka madhara yake.

Hata wanapojikinga, watu wanafaa kuepuka kuwasha meko ya makaa ndani ya nyumba zao bila hewa ya kutosha kwa sababu yanaweza kusababisha madhara makubwa kikiwemo kifo.

Wataalamu wanashauri watu kuvaa mavazi yenye joto na kutumia vyakula vya kuongeza joto katika miili yao.Ni muhimu kukumbuka kuwa daima kinga na bora kuliko tiba.

Hivyo basi watu wanafaa kutii ushauri huu wa wataalamu ili wasijitumbukize katika hasara ambayo wanaweza kuepuka hasa wakati huu gharama ya matibabu inapoendelea kupanda sawa na gharama ya maisha.

Wizara ya Afya pia imeonya watu kuwa msimu wa baridi unaweza kusababisha mkumbo mwingine wa virusi vya Covid-19.

Hakuna anayetaka hali kurudi ilipokuwa miaka miwili iliyopita, virusi hivyo vilipolemaza kila sekta ya uchumi.

Kuepuka hali hii ni rahisi; kila mmoja azingatie kanuni za kujikinga na kukinga wengine ambazo ni kuvaa maski, kudumisha usafi binafsi na kupata chanjo inayotolewa bila malipo na serikali.

Baridi kali ni hatari na kuepuka hatari hiyo kunahitaji mtu kuwajibika binafsi na kwa wapendwa wake.

You can share this post!

Washirika wa Ruto wazidi kuponda Uhuru

Rais ahepa ghadhabu za raia

T L