• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Washirika wa vigogo wasisitiza mwaniaji wao ndiye astahili

Washirika wa vigogo wasisitiza mwaniaji wao ndiye astahili

Na WANDERI KAMAU

WASHIRIKA wa karibu wa vigogo hao wanawataja kuwa watu wenye maono, na viongozi bora zaidi kuiongoza nchi kutokana na tajriba yao kubwa kwenye siasa.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro anamtaja Naibu Rais William Ruto kuwa mwenye ufahamu mpana kuhusu changamoto zinazowakumba Wakenya.

“Ruto ni mwanasiasa ambaye safari yake ni wazi kuhusu alikoanzia hadi alikofika. Ni kiongozi aliyejiinua kimaisha kutoka kuwa muuzaji kuku hadi akawa naibu rais. Ikilinganishwa na wale wengine, yeye ndiye mwenye ufahamu mzuri zaidi kuhusu matatizo yanayomkumba Mkenya wa kawaida. Huo ndio mwongozo wa mrengo wa ‘Hustler Nation’, ambao ni kuwainua wananchi wa chini kiuchumi,” akasema Bw Nyoro.

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed anamtaja Kinara wa ODM, Raila Odinga kuwa kiongozi ambaye amejitoa kafara katika maisha yake kwa ajili ya uthabiti wa kisiasa nchini na kutetea mwananchi.

“Bw Odinga hawezi kulinganishwa na mwanasiasa yeyote yule hapa Kenya. Ni kiongozi aliyeonyesha ukakamavu mkubwa licha ya changamoto za kisiasa ambazo zimekuwa zikimwandama. Kwa mfano, hatua yake kubuni handisheki ilikuwa kuona hali ya utulivu imerejea nchini, wala si kwa manufaa yake binafsi,” akasema Bw Mohamed.

Mbunge Dan Maanzo (Makueni), ambaye ni mshirika wa karibu wa Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka anamsifu kuwa kiongozi mvumilivu na muungwana.

“Ni kupitia unyenyekevu wa Bw Musyoka kukubali kuwa Makamu wa Rais wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki 2008 ndipo nchi ilitulia. Vile vile, amewaunga mkono wanasiasa wengine kuwania urais mara mbili. Huu ni wakati wake. Naamini ana suluhisho bora kwa matatizo yanayoikumba nchi,” akasema.

You can share this post!

Afisa wa polisi aliyetoweka mwaka mmoja uliopita bado...

DPP kumshtaki afisa wa polisi kwa mauaji ya bucha Kiamaiko