• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Watoto wa Raila, Kalonzo watoa vilio kwa wabunge

Watoto wa Raila, Kalonzo watoa vilio kwa wabunge

NA WAANDISHI WETU

BINTIYE kiongozi wa ODM Raila Odinga, Winnie Odinga na mwanawe kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Kennedy Musyoka wamelilia wabunge kuwachagua kuingia bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Wawili hao walizungumza wakirai wabunge kuwapigia kura katika uchaguzi wa Novemba 17, 2022 bungeni.

Wawili hao walisema wanafaa kutazamwa kama Wakenya kwa kutegemea ufaafu wao bila kujali familia wanazotoka.

Bi Odinga alisema azma yake katika EALA haina uhusiano na baba yake, akisema anafanya kampeni kama wengine waliopendekezwa na majina yao kuwasilishwa bungeni.

Bw Musyoka, aliyehudumu kwa miaka mitano katika EALA, alisema tajiriba yake ya miaka mitano inampa uwezo wa kuendelea kuhudumu.

Wakati huo huo, Rais William Ruto wiki ijayo ataongoza kikao cha nne cha wabunge wa Kenya Kwanza (PG) kuwakabidhi chaguo lake la wanachama wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

“Kabla ya kuamua wale watakaochaguliwa kwa nyadhifa tano tulizo nazo katika EALA, mkubwa ameitisha kikao cha wabunge wiki ijayo kujadili suala hilo. Katika kikao cha wabunge kilichopita, tulikubaliana kuhusu Kamati tofauti, alikuwa ameahidi kukutana nasi tena kuhusu suala la EALA,” alisema mmoja wa washirika wa karibu wa Rais Ruto.

Kenya Kwanza imeteua watu 15 kwa uchaguzi wa EALA, ambao ni aliyekuwa seneta wa kuteuliwa David Sankok na Hassan Omar.

Wengine ni Yasser Bajaber, Salim Busidy, Lilian Tomitom, Cyprian Iringo, Jonas Kuko, Abdikadir Aden na Falhadha Iman.Joel Nyambane, Godfrey Karobia, Fredrick Muteti Charles, Zipporah Kering, na Rebecca Lowoiya pia wanamezea mate nyadhifa hizo tano.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Sakaja aanza mbio kutekeleza agizo la mke wa Rais

Majambazi wateka miji na vijiji nchini

T L