• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:55 AM
Wawaniaji huru tisa kumkabili ‘Jicho Pevu’

Wawaniaji huru tisa kumkabili ‘Jicho Pevu’

NA VALENTINE OBARA

ENEOBUNGE la Nyali lina idadi kubwa zaidi ya wagombeaji huru waliojiandikisha kutaka kushiriki katika uchaguzi wa Agosti.

Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), eneobunge hilo linalosimamiwa na Bw Mohamed Ali, almaarufu kama Jicho Pevu, limevutia wawaniaji huru tisa wanaosubiri kuidhinishwa.

Bw Ali alishinda kiti hicho 2017 kama mwaniaji huru aliyeegemea upande wa kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.

Wakati huu, amejiunga na Chama cha UDA kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Mwaka wa 2017, Nyali kulikuwa na wawaniaji ubunge 14 ambapo wawili pekee ndio walikuwa wa kujitegemea.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, wawaniaji huru waliopita awamu ya kwanza watahitajika kufika mbele ya maafisa wakuu wa uchaguzi katika maeneo yao kabla wateuliwe rasmi.

“Wataitwa kuhudhuria mikutano katika tarehe zitakazotangazwa baadaye ili wafahamishwe kuhusu mahitaji wanayofaa kutimiza kabla kuwa wawaniaji katika uchaguzi wa Agosti,” Bw Chebukati alieleza.

Eneobunge lingine ambalo limevutia idadi kubwa ya wawaniaji huru ni Likoni.

Wawaniaji huru saba wanataka kuteuliwa na IEBC kushindania kiti hicho kinachokaliwa na Bi Mishi Mboko wa Chama cha ODM.

Katika eneobunge la Kisauni, wanasiasa sita wanataka kushindania urithi wa kiti cha Bw Ali Mbogo, kama wawaniaji huru.

Bw Mbogo hatatetea wadhifa wake kwani Chama cha Wiper kilimteua kuwa mgombea mwenza wa gavana wa zamani wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kwa shindano la ugavana Mombasa.

Awali alitaka kuwania ugavana.Eneobunge la Mvita ambalo pia litabaki wazi kwa vile mbunge wake, Bw Abdulswamad Nassir, anawania ugavana kupitia ODM, limevutia wawaniaji huru watatu.

Idadi sawa na hiyo iko Changamwe, huku Jomvu kukiwa na wawili pekee.

Katika Kaunti ya Kwale, eneobunge la Msambweni limevutia wawaniaji huru wanne, huku kukiwa na watatu Kinango na mmoja Matuga.

Eneobunge la Kilifi Kusini, Kaunti ya Kilifi, lina wawaniaji huru watano likifuatwa na Kaloleni (watatu), Rabai (wawili), Magarini (wawili), Ganze na Malindi mmoja mmoja.Maeneobunge ya Taita Taveta na Tana River hayana wawaniaji huru zaidi ya wawili katika maeneobunge, huku Lamu kukikosekana.

Mbali na hayo, imebainika wawaniaji huru wengi Pwani wamekwepa kinyang’anyiro cha ugavana, useneta na uwakilishi wa wanawake bungeni.

Hii ni baada ya wengi waliokosa tikiti za vyama vikubwa kuwania nyadhifa hizo kuamua kujiunga na vyama vidogo au kupumzisha maazimio yao ya kisiasa.

Kaunti ya Taita Taveta imevutia wawaniaji huru watatu akiwemo Mbunge wa Mwatate, Bw Andrew Mwadime, huku kukiwa na mmoja mmoja Mombasa na Kwale.

Kwa useneta, Kaunti ya Mombasa imevutia watatu akiwemo Bw Mohamed Amir ambaye ni kakake Gavana Hassan Joho.

Bw Amir alihama Chama cha UDA baada ya kukosa kupewa tikiti.

Kaunti za Kwale, Taita Taveta na Lamu zina wawaniaji huru mmoja mmoja, akiwemo Seneta wa Lamu, Bw Anwar Loitiptip.

Idadi ya wawaniaji huru wanaotaka kiti cha mwakilishi wa kike bungeni pia ni ndogo Pwani ambapo kuna watatu Mombasa, na mmoja mmoja Kwale, Kilifi, Lamu na Taita Taveta.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool yasuka njama ya kupokonya City windo la EPL

Boga sasa abadili mgombea mwenza

T L