• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wawaniaji huru wa urais ni vibaraka wa serikali – Mudavadi

Wawaniaji huru wa urais ni vibaraka wa serikali – Mudavadi

NA WYCLIFFE NYABERI

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amedai huenda idadi kubwa ya wawaniaji huru wanaokitafuta kiti cha urais ikawa njama ya watu fulani wanaotumiwa kisiri kugawanya kura za urais.

Mudavadi, aliyatamka hayo Alhamisi kwenye kongamano la kiuchumi katika kaunti ya Nyamira, eneo la Nyamaiya, lililoandaliwa na Naibu Rais Dkt William Ruto na viongozi wengine wa muungano wa Kenya Kwanza.

Bw Mudavadi alieleza licha ya kuwa wawaniaji hao wana haki yao ya kidemokrasia kikatiba, Wakenya wanafaa kuwa makini nao kwani katika historia ya Kenya na ndani ya katiba ya mwaka 2010, hakujawahi shuhudiwa idadi kama hiyo ya juu ya wawaniaji wanaosaka kura ya urais bila vyama.

Baada ya kumalizika kwa makataa ya Afisi ya Msajili wa Vyama kwa wawaniaji huru kuwasilisha stakabadhi zao, ilibainika kuwa watu zaidi ya 45 walikuwa wakisaka kumrithi rais Uhuru Kenyatta bila kutumia vyama kwenye uchaguzi wa mwezi Agosti.

“Hakujawahi shuhudiwa idadi ya juu kama iliyo sasa kuhusu wawaniaji huru wanaomezea mate kiti cha urais. Lazima tuliangalie hili kwa umakinifu kwani huenda kukawa na njama ya kugawa kura za watu fulani na baadhi ya watu. Msikubali hilo,” Bw Mudavadi akasema.

Kwa siku mbili zilizopita, Muungano wa Kenya Kwanza umekuwa ukikita kambi katika kaunti za Kisii na Nyamira.

Naibu Rais amekuwa akiwaskiza wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusu yale wangependa awafanyie ikiwa atafaulu kuingia Ikulu.

Kama ilivyo ibada yake, Dkt Ruto alijisifia miradi mbali mbali iliyofanikishwa na serikali ya Jubilee licha ya mafarakano yanayoshuhudiwa kwa sasa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Miradi hiyo ni barabara za lami, kuunganisha Wakenya na umeme, ujenzi wa vyuo anuwai na kadhalika.

Huku akiwapa wapiga kura ahadi tele, Naibu Rais alisema sekta za kilimo, juakali, mama mboga na bodaboda ndizo atakazozipa kipaumbele akitwaa uongozi wa taifa.

Dkt aliahidi kuweka mikakati itakayowainua watu wa chini hadi viwango vya juu kama unavyopendekeza mfumo wake wa Bottom Up, huku akisemezana moja kwa moja na baadhi ya waliochaguliwa kuwakilisha wananchi.

Kuhusu kinyang’anyiro cha urais, Naibu Rais alisema safari hii haitakuwa kuhusu namna watu fulani watagawana vyeo na kubadilisha katiba bali kubadili uchumi wa taifa hili kwa sera mahususi zinazolenga watu wa matabaka ya chini.

“Kama serikali ya Kenya kwanza, tutakuwa na mpango maalum wa kubuni nafasi za ajira ili vijana wetu wajitegemee wenyewe. Tutapanga biashara zenu na kilimo chenu ikiwa mtakubali tushirikiane,” Dkt Ruto akasema.

Ikiwa atafaulu kuwa rais wa tano wa taifa, Dkt Ruto alisema ifikapo Desemba, watahakikisha kila Mkenya anapata bima ya taifa ya matibabu.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Askofu Anthony Muheria: Nahodha...

Pigo kwa uchumi pato la kilimo likishuka mno

T L