• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Wawaniaji Mlima Kenya wahofia kupokonywa tikiti ndani ya Azimio

Wawaniaji Mlima Kenya wahofia kupokonywa tikiti ndani ya Azimio

NA MWANGI MUIRURI

WAWANIAJI wa viti mbalimbali kupitia vyama tanzu vya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya katika eneo la Mlima Kenya wameingiwa na wasiwasi baada ya kufahamishwa kuwa baadhi yao watapokonywa tikiti kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Mgombeaji wa Urais kwa tiketi ya muungano huo Raila Odinga alisema kuwa wanalenga kuwasimamisha wagombeaji ambao matokeo ya kampuni mbalimbali za utafiti yatawaonyesha kama wanaojivunia umaarufu mkubwa wa kisiasa.

“Ikiwa imesalia miezi miwili tutathmini iwapo wawaniaji ambao wana tiketi za vyama vyetu na kuhakikisha kuwa wale ambao wanafika debeni ni wale ambao ni maarufu. Hatutaki vyama tanzu ndani ya Azimio viwe na wawaniaji wengi ambao watagawa kura kisha kuwapa wapinzani wetu ushindi,” akasema Bw Odinga katika hoteli ya Thika Greens Hotel.

Kauli ya Bw Odinga imewakasirisha baadhi ya wawaniaji wa vyama tanzu ambao wanahofia kuwa huenda wasifike debeni licha ya kutwaa tikiti za vyama vyao baada ya kushinda uteuzi.

Mwenyekiti wa Kundi la Madiwani kutoka Ukanda wa Mlima Kenya Charles Mwangi alisema Bw Odinga alisukumwa atoe kauli hiyo na Jubilee ambayo inalenga kuhakikisha vyama vingine tanzu havisimamishi wawaniaji eneo hilo.

Kutokana na usemi huo wa Bw Odinga, mwaniaji wa kiti cha ubunge wa Kandara, Julius Kaberere alitangaza kuwa amejiondoa katika chama hicho na sasa atagombea kama mwaniaji huru.

Naye Mbunge wa Gatanga Nduati Ngugi alisema kuwa itakuwa vigumu kuwashurutisha wawaniaji wa vyama vingine wajiondoe kwa sababu wamewekeza katika kampeni zao na iwapo hilo litafanyika basi lazima itakuwa Juni kabla ya majina kuchapishwa kwenye karatasi za kura.

Katika Kaunti ya Tharaka-Nithi wawaniaji wakuu wa kiti cha ugavana wamesimama kidete kuwa lazima wafike debeni baada ya kusambaratika kwa juhudi za kuwataka waungane chini ya Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Aliyekuwa Chansela wa Chuo Kikuu cha Chuka Profesa Erastus Njoka (Jubilee), Dkt Mzalendo Kibunjia (Narc Kenya) na Nyamu Kagwima wa Wiper, wote wamesisitiza kuwa watawania kiti hicho. Msimamo wao sasa unadidimiza matumaini ya Azimio kushinda kiti hicho.

Duru zinaarifu kuwa juhudi za Rais Uhuru Kenyatta kumtaka Dkt Kibunjia amuunge mkono Profesa Njoka zimeambuliwa patupu. Rais Kenyatta wiki mbili zilizopita alimteua mgombeaji mwenza wa Dkt Kibunjia Jane Kithinji kama balozi wa Kenya kule Moscow, Urusi.

  • Tags

You can share this post!

Sasa yabainika Sankok anamiliki bastola mbili

WANDERI KAMAU: Askofu Anthony Muheria: Nahodha...

T L