• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wazee wafanya Rais ajikune kichwa zaidi

Wazee wafanya Rais ajikune kichwa zaidi

NA WAWERU WAIRIMU

RAIS Uhuru Kenyatta anakabiliwa na kibarua kigumu kuliunganisha eneo la Kaskazini Mashariki ili kumsaidia kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kupata kura zaidi ya 800,000 miongoni mwa wenyeji kwenye uchaguzi wa Agosti.

Hii ni baada yake kuelezea kutoridhishwa na mfumo wa makubaliano kuhusu viongo – zi watakaochaguliwa, ambao huendeshwa sana katika eneo hilo.

Tayari, Rais Kenyatta ametangaza anamuunga mkono Bw Odinga kuwa mrithi wake.

Wazee kutoka jamii nyingi za kuhamahama tayari wamekutana na kukubaliana kuhusu viongozi watakaochaguliwa kwa nafasi mbalimbali za kisiasa.

Kwa siku tatu zilizopita, Rais Kenyatta amekutana na wajumbe kutoka kaunti za Marsabit, Tana River, Mandera na Isiolo.

Kwenye vikao hivyo, amekuwa akisisitiza kuhusu haja ya viongozi wote kupewa nafasi sawa kwa nyadhifa wanazolenga kuwania.

Alipokutana na viongozi wa Kaunti ya Marsabit, wakiongozwa na Waziri wa Fedha Ukur Yatani na mbunge Chachu Nganya, Rais Kenyatta alieleza wazi kuwa lazima jamii zote zipewe nafasi za uwakilishi katika kaunti na ngazi ya kitaifa.

“Hata ikiwa mtamchagua Mrendille, Mgabbra, Mborana, Msakuye au mtu kutoka jamii nyingine, lazima pawe na uwakilishi kutoka pande zote,” akasema Rais Kenyatta, kwenye hotuba iliyoonekana kukosoa mfumo huo.

Duru zilisema kuwa kauli ya Rais ilitokana na malalamishi kutoka kwa baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo kwamba baadhi ya jamii zimekuwa zikitengwa kwenye masuala ya uongozi.

Inadaiwa Rais Kenyatta aliambiwa kuwa huenda malalamishi hayo yakaathiri mipango ya kuwarai wenyeji kumuunga mkono Bw Odinga.

Baadhi ya wakazi na wawaniaji wamejitokeza kuukosoa mfumo huo, wakisema umekuwa ukiwazuia kutimiza ndoto zao za kisiasa. Wamekuwa wakidai pia umetumiwa kuyatenga baadhi ya makundi katika jamii kama walemavu.

Mfumo huo umekuwa ukionekana kama njia ya kuzua ghasia zinazohusiana na masuala ya siasa, hasa nyakati za uchaguzi.

Jamii ndogo zimekuwa zikilalamika kuwa mfumo huo umekuwa ukizipendelea jamii kubwa pekee. Zinashikilia ni hali ambayo huenda ikavuruga uthabiti wa kisiasa ambao umekuwepo.

Katika Kaunti ya Isiolo, kwa mfano, hatua ya jamii ya Waborana kutengewa nafasi za Gavana, Seneta, wabunge na Mwakilishi wa Kike, imezua hisia mseto miongoni mwa jamii ndogo.

Wazee waliwapa aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Godana Doyo, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti Mohammed Tupi na Bw Nuh Mohammed Ibrahim mtawalia ‘baraka’ za kuwania ugavana, ubunge katika eneo la Isiolo Kusini na useneta mtawalia.

Wazee hao pia waliwapa Mwakilishi wa Kike, Rehema Jaldesa na mbunge Hassan Odha (Isiolo Kaskazini) uhuru wa kutetea viti vyao tena.

Hata hivyo, hatua hiyo imepuuziliwa mbali na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Halakhe Waqo na aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Bi Mumina Bonaya.

  • Tags

You can share this post!

ODM yaonya wanasiasa wake dhidi ya kuzua vurugu

Matumizi ya trei kukuza miche ya mahindi hasa maeneo kame

T L