• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Matumizi ya trei kukuza miche ya mahindi hasa maeneo kame

Matumizi ya trei kukuza miche ya mahindi hasa maeneo kame

Na SAMMY WAWERU

MABADILIKO ya tabianchi ni wazi kufuatia athari zake zinazoendelea kutatiza maeneo mbalimbali nchini.

Ukame na kiangazi, umekuwa kero kwa zaidi ya kaunti 20 mimea na mifugo ‘ikisaliti amri’. Kaunti za jamii ya wafugaji na ambazo zimekodolewa macho na hatari ya ukame, zimekadiria hasara ya mifugo kufa njaa.

Mimea imekauka, wakazi wakitegemea chakula cha msaada kutoka kwa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile; Shirika la Chakula na Kilimo la UN – FAO, kati ya mengineyo.

Mche wa mahindi uliooteshwa (mbegu) na kukuzwa kupitia teknolojia ya trei…Picha/SAMMY WAWERU

Nchi zilizo katika Upembe wa Afrika (Horn of Africa), ni miongoni mwa zilizoathirika kwa kiasi kikuu ulimwenguni na upungufu na ukosefu wa chakula. FAO, imetaja Kenya, Ethiopia na Somalia kama nchi zilizoathirika pakubwa, takwimu zikionyesha watu milioni 25.3 watakumbwa na baa la njaa kufikia Juni mwaka huu hali ikiendelea inavyoshuhudiwa.

Tayari shirika hilo limepuliza kipenga, likiomba msaada wa dharura kusaidia watu milioni 1.5 wanaoishi maeneo ya mashambani Pembe ya Afrika. Aidha, FAO imesema kima cha Dola 138 milioni zinahitajika kuendesha oparesheni hiyo, ikionya huku awamu ya tatu ya ukame ikibisha hodi huenda mambo yakawa mabaya zaidi endapo jamii zilizoathirika hazitaokolewa.

Urbanus Kamuti na wakulima wenza waliokumbatia teknolojia ya trei kuotesha mbegu za mahindi kupata miche…Picha/SAMMY WAWERU

Mambo yakizidi unga, wakulima katika kaunti kame wanahimizwa kukumbatia mifumo itakayowezesha uzalishaji mfululizo wa chakula. Kaunti ndogo ya Mwala, Machakos, ni kati ya maeneo yanayokumbwa na janga la kiangazi.

Hata hivyo, Urbanus Kamuti, mkazi anaelewa bayana manufaa ya teknolojia za kilimo maeneo kame. Ana bwawa dogo, linalovuna maji msimu wa mvua. Ni kutokana na ubunifu wake shamba lake ni mithili ya mabustani Israili.

Uwe msimu wa mvua au ukame, hutakosa kuona mahindi yaliyonawiri. Kamuti anasema mfumo wa trei umefanikisha hatua hiyo. Wakulima wa nafaka wamekumbatia upanzi wa mbegu za mahindi moja kwa moja kwenye mashimo.

Kamuti hata hivyo hutumia trei kuotesha na kukuza miche, ambayo huchukua kati ya majuma matatu au manne, sawa na mwezi mmoja kukomaa – tayari kuhamishiwa shambani.

“Msimu wa mvua unapobisha hodi, mkulima apande miche kwenye trei mwezi mmoja kabla,” ahimiza mkulima huyo. Aidha, ana jumla ya trei 50. Trei ina vijishimo vya kupanda mbegu, ambapo hutumia mbolea asili, ikiwemo ya mifugo na mboji/vunde-mchanganyiko wa mimea iliyooza.

Idadi ya mashimo inalingana na ukubwa wa trei, nyingi zikiwa na kati ya 100 – 300. Mfumo wa trei unafanikisha asilimia 100 ya uotaji wa mbegu kuwa miche. Kamuti huitunzia kenye kivungulio cha neti, kilichozingirwa ili kuepushia miche maadui kama mifugo na nguchiro.

“Nguchiro na panya huharibifu mbegu sana kabla ziote na kuchipuka,” asema. Pius Opiyo, mtaalamu kutoka ACE Agriculture anasema mfumo wa trei kando na kuhakikisha miche ni salama, huokolea mkulima muda.

oise Ndung’u (aliyevalia sweta nyeusi) akifunza wakulima kuhusu matumizi ya trei kuotesha mbegu za mboga kuwa miche…Picha/SAMMY WAWERU

“Hasara inayotokana na mvua kuchelewa, mbegu kuozea shambani na kushambuliwa na adui wa nafaka, matumizi ya trei yanaiondoa,” Opiyo asema, akishauri wakulima kuukumbatia.

Mbali na mahindi, trei pia hutumika kuotesha mbegu za mboga, nyanya na vitunguu. Loise Ndung’u, mkuzaji wa miche ya mboga na nyanya Kaunti ya Murang’a amekumbatia mfumo huo.

“Ni bora kuliko tuta. Huwa na uhakika wa asilimia 100 kwa 100 mbegu kuota kuwa miche,” Loise aelezea, akifisifia mfumo huo. Urbanus Kamuti naye anasema ni kutokana na manufaa chungu nzima ya teknolojia ya trei huweza kuwa na mavuno kila wakati, biashara yake ikiwa ni ya mahindi mabichi.

Ni mfumo ambao wakulima wakiitikia kuutumia, hasa katika maeneo kame na jangwani, huenda kero ya upungufu na ukosefu wa chakula itaangaziwa. Itakuwa busara wakifumbua macho na kujua namna na mifumo faafu kiteknolojia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hali ya anga imebadilika, na kusambaratisha misimu ya mvua Kenya.

Miche ya mbegu inayozalishwa kupitia trei…Picha/SAMMY WAWERU

You can share this post!

Wazee wafanya Rais ajikune kichwa zaidi

Kibarua akana kuiba Vaseline

T L