• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Zogo ODM ikimpa Boga tiketi mboga Kwale

Zogo ODM ikimpa Boga tiketi mboga Kwale

NA SIAGO CECE

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinakabiliwa na mzozo mkubwa katika kaunti ya Kwale baada ya chama hicho kumpa tikiti ya moja kwa moja aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kilimo Prof Hamadi Boga kugombea kiti cha ugavana cha kaunti hiyo.

Uamuzi huo umezua joto kubwa huku baadhi ya wafuasi wake wakipanga kukihama chama hicho wakidai hakina usawa.

Kulingana na Mwenyekiti wa ODM kaunti ya Kwale Hassan Mwanyoha, chama hicho kilifikia uamuzi huo ‘kufuatia maagizo kutoka kwa afisi ya juu zaidi’.

“Profesa Boga ndiye amepewa tikiti. Hili lilikuwa ni agizo kutoka afisi ya juu zaidi na ilibidi tulifuate,” Bw Mwanyoha aliambia Taifa Jumapili kwenye mahojiano.

Profesa Boga sasa atakuwa kwenye debe na mgombea mwenza Safina Kwekwe.

Chama cha ODM kilikuwa kimewavutia wagombeaji wanne akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa ODM Agnes Zani, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kwale Sammy Ruwa na aliyekuwa Mhandisi wa Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) Chai Lung’anzi.

Bw Mwanyoha alisema kuwa Bw Ruwa alikuwa mtu wa kwanza kujiondoa kwenye chama na kuhamia chama cha Gavana wa Kilifi Amason Kingi, Pamoja Africa Alliance (PAA).

Walio karibu na Bw Lung’anzi wamesema kuwa pia anatafuta nafasi katika chama cha PAA baada ya kunyimwa tikiti ya chama cha ODM.

“Lengo letu ni Agosti 9, tutatoa msimamo wetu haraka iwezekanavyo,” alichapisha kwenye mitandao yake ya kijamii siku moja baada ya Profesa Boga kukabidhiwa tikiti.

Mapema mwaka huu 2022, alikuwa amedokeza kwamba ingawa alikuwa na matumaini ya kupata tikiti, angemuunga mkono Profesa Boga ikiwa mmoja wao atapata uteuzi.

Lakini wiki jana aliambia Taifa Jumapili kuwa hawezi kujiunga na Bw Boga kwani wote ni washindani.

Awali Bw Lung’anzi alikuwa amejiondoa kutoka kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) baada ya kuhisi kushindwa wakati Mgombea Urais wa chama hicho Naibu Rais William Ruto alipotembelea Kaunti ya Kwale na kumwidhinisha Naibu Gavana wa Kwale Fatuma Achani.

Profesa Boga, ambaye hivi majuzi alijiuzulu serikalini sasa atatarajiwa kumenyana na Bi Achani ambaye ndiye mgombeaji pekee wa UDA, aliyekuwa Balozi Chirau Ali Mwakwere wa Wiper na mfanyabiashara Gereza Dena wa KANU.

Wiki jana Profesa Boga aliomba apewe tikiti ya chama hicho kwa sababu ya umaarufu wake katika chama, na hata akamrushia ndoana Bw Lung’anzi akimtaka kuungana naye ili wafanye kazi pamoja kabla kura za uteuzi.

Lakini kuteuliwa kwa Prof Boga kunaleta kitendawili kikubwa huko Kwale kwani ikiwa Bw Lung’anzi atagombea kwa chama kingine, hii itamaanisha kuwa atagawanya kura za Waduruma, ambako yeye ni maarufu kwa sababu anatoka jamii hiyo.

Bi Achani na Profesa Boga wote wanatoka katika jamii ya Digo ambao ni wachache.

Jamii nyingine za Kwale ni Wakamba ambao wamemiliki sehemu za Lungalunga na Kinango.

Takriban miaka miwili iliyopita, chama cha ODM kilipoteza kiti baada ya kumuunga mkono, Omar Boga, ambaye alishindwa na Feisal Bader, mgombeaji huru wa kiti cha ubunge wa Msambweni katika uchaguzi mdogo baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Msambweni marehemu Suleiman Dori.

Bw Mwanyoha hata hivyo hakudokeza ikiwa mfumo sawa na uliotumiwa kwenye ugavana utatumiwa kwa wagombea katika nafasi ya useneta, Uwakilishi wa Wanawake na nafasi ya ubunge.

You can share this post!

TAHARIRI: Pombe haramu ni janga kwa taifa letu

BAHARI YA MAPENZI: Gharama ya ndoa

T L