• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:40 PM
Zuleikha apinga ushindi wa Mwanyoha uenyekiti ODM

Zuleikha apinga ushindi wa Mwanyoha uenyekiti ODM

Na SIAGO CECE

MZOZO umeibuka baada ya uchaguzi wa tawi la Kwale la chama cha ODM kati ya aliyekuwa mbunge wa Matuga Hassan Mwanyoha na Mwakilishi wa Wanawake Bi Zuleikha Hassan.

Bi Hassan alipinga matokeo ambayo Bw Mwanyoha alichaguliwa mwenyekiti wa tawi hilo akisema wajumbe wote hawakushirikishwa kwenye uchaguzi huo.

Bi Hassan na wanaomuunga mkono wanataka makao makuu ya ODM kukataa matokeo ya uchaguzi huo.

Mbunge huyo ambaye alikuwa akiwania kiti cha mwenyekiti alisema kwamba uchaguzi haukufanyika vyema na kwamba afisa aliyeusimamia ni mfanyakazi wa Bw Mwanyoha.

Aliongeza kuwa Bw Swaleh Guyo hakutambuliwa na Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya ODM na kwa hivyo hakufaa kusimamia uchaguzi huo.

Bw Said Mwanauba, ambaye ni mfuasi wa Bi Hassan alidai kuwa baadhi ya wajumbe hawakuhusishwa kuupanga.

“Tunapinga matokeo ya uchaguzi kwa kuwa kila mtu hakushiriki. Tulikuwa tumepanga kuwa na uchaguzi wa siri ili uwe huru na wa haki,” alisema Bw Said.

Kundi hilo sasa linataka viongozi chama cha ODM kutoidhinisha majina ya viongozi waliochaguliwa na kupanga uchaguzi mwingine katika kaunti hiyo ambao utakuwa wa siri.

Chama hicho kilisema kwamba uchaguzi wa mashinani unafaa kuwa wa muafaka ili kila mtu akubali viongozi.

Hata hivyo, Bw Mwanyoha ambaye ni mwenyekiti mteule wa tawi hilo alisema uchaguzi huo ulikuwa wa haki kwa kuwa kanuni za uchaguzi za chama zilizingatiwa.

“Tulifanya uchaguzi wetu kupitia muafaka kwa kujaza viti vilivyokuwa wazi na watu waliohama au kufariki au wagonjwa. Mwanyoha hakuhama, sio mgonjwa na hajakufa,” alisema Mwanyoha.

Alisisitiza kuwa wajumbe wote wa tawi la ODM kaunti ya Kwale walikubaliana mbinu ya kuandaa uchaguzi kwenye mkutano na viongozi kutoka makao makuu ya chama.

Alisema kwamba uchaguzi kupitia muafaka ulikuwa wa kujaza nafasi zilizokuwa wazi kufuatia wanachama kuhama chama hicho au kufariki.

Wanachama wengi wa ODM kaunti ya Kwale wamefariki tangu uchaguzi mkuu wa 2017.

You can share this post!

Afueni bei ya kahawa ikiimarika

Tahadhari yatolewa kuhusu vifaa ghushi vya kupima Ukimwi