• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Maridhiano ‘yapiga hatua’ Azimio wakikubali kushiriki mapumziko ya wiki nzima Nakuru

Maridhiano ‘yapiga hatua’ Azimio wakikubali kushiriki mapumziko ya wiki nzima Nakuru

NA LABAAN SHABAAN

SHUGHULI za Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo ya Maridhiano (NADCO) zinaonekana kupiga hatua.

Hii ni kufuatia Muungano wa Azimio la Umoja kukubali kushiriki mapumziko katika mkahawa wa Lake Elementaita Mountain Lodge, Kaunti ya Nakuru, kujadili mbinu ya kuwasilisha ripoti.

Haya yanajiri baada ya atiati kuibuka Azimio walipotishia kutoshiriki kikao cha kuandaa ripoti iwapo suala la gharama ya maisha halitaangaziwa.

Wanakamati wa NADCO walionekana wakiwasili kwa pumziko hilo Jumatatu Oktoba 23, 2023.

Wawakilishi wa Serikali ya Kenya Kwanza waliongozwa na mwenyekiti-mwenza Kimani Ichung’wah kushiriki hatua za lala salama za machakato wa maridhiano.

Pamoja na Bw Ichung’wa, wanakamati wa serikali waliofika hotelini ni Kiongozi wa Wengi wa Seneti Aaron Cheruiyot na Gavana wa Embu Cecily Mbarire.

Wajumbe wa Upinzani waliotaataa awali pia walifika mkahawani humo ulioko eneobunge la Gilgil.

Waliofika ni Kiongozi wa Wachache wa Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi na Kinara wa Azimio  Eugene Wamalwa.

Mwenyekiti-mwenza wa NADCO anayewakilisha Azimio Kalonzo Musyoka na wanachama wengine waliwasili baadaye.

Katika kikao hiki cha wiki moja, kamati hii itachambua hoja zilizowasilishwa na washikadau mbalimbali katika vikao vilivyofanyika ukumbini Bomas jijini Nairobi.

Vikao vya Bomas vilitamatika Oktoba 6, 2023.

Mnamo Oktoba 22, 2023 Kiongozi wa Azimio Raila Odinga alisema hatatia sahihi ripoti ya NADCO kama haitaorodhesha kushusha gharama ya juu ya maisha kuwa kipaumbele.

“Tunazungumza na serikali lakini suala la kwanza lazima liwe kupunguza gharama ya maisha,” Bw Odinga alisema.

Wakati huo huo, Upinzani umekuwa ukimshinikiza Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula kumvua Bi Sabina Chege mamlaka ya Kiranja wa Wachache bungeni kwa sababu ya kuunga serikali na hali yeye ni mwanachama wa Azimio.

“Hatutahudhuria mkutano huo ikiwa hawatatekeleza uamuzi wa kumng’oa Sabina Chege kutoka wadhifa huo,”  Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni aliambia Taifa Leo akieleza mojawapo ya majukumu ya kamati ya mazungumzo ni kuhakikisha kanuni za vyama zinafuatwa.

Muungano huo umeamua Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje achukue nafasi ya Bi Chege, lakini uamuzi huo bado haujatekelezwa.

Kamati hiyo tayari imeafikiana kuhusu masuala muhimu ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi kipya cha kuteua mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na makamishna sita.

Miezi sita baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, upinzani ulitangaza maandamano dhidi ya serikali.

Maandamano hayo yalisababisha vifo vya watu 75 na uharibifu wa mali ya mamilioni ya pesa.

Mikasa hii ilisukuma pande hizi mbili kuafikiana na kuunda kamati ya maridhiano.

Ukaguzi wa kura za urais, mchakato wa uteuzi wa tume mpya ya uchaguzi na gharama ya maisha yalikuwa baadhi ya malilio ya Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Mama yangu anapanga kuolewa na ‘Ex’ wangu

Haitawezekana wahubiri kuwa na digrii – Maina Njenga

T L