• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Haitawezekana wahubiri kuwa na digrii – Maina Njenga

Haitawezekana wahubiri kuwa na digrii – Maina Njenga

NA FRIDAH OKACHI

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi la Mungiki Maina Njenga, amepinga hatua ya serikali ya Kenya Kwanza kutaka wahubiri kuwa na cheti cha shahada.

Bw Njenga ambaye ni Mhubiri wa Kanisa la Hope International Ministry, alisema itakuwa vigumu wahubiri kuwa na stakabadhi hiyo akirejelea wito wa viongozi wa dini kuchunguzwa na serikali kutambua iwapo wahubiri wamehitimu.

Aliyekuwa Kiongozi wa Kundi la Mungiki, Maina Njenga. Picha|Maktaba

“Kuwa na Shahada haitawezekana, Yesu hakuwa na cheti cha kuongoza wafuasi wake. Wokovu hauhitaji cheti,” alihoji.

Kiongozi huyo ametaka wahubiri kulipa ushuru akisema kueneza injili ni kama kazi nyingine yoyote ambayo wahubiri hupata mapato ya sadaka.

“Watu wakubali kutoa ushuru. Kanisa haliwezi kusimama bila sadaka na serikali haiwezi kufanya shughuli zake bila ushuru,” alisema Bw Njenga.

Akihojiwa kwenye kituo kimoja cha redio humu nchini, Mhubiri Njenga amekana madai ya kujificha kwenye dini na wokovu.

Alianza kuhudumu kwenye kanisa lake mwaka 2005 baada ya kupelekwa kwenye jela la Kamiti na kukaa miaka miwili akisoma biblia.

Njenga alitumikia miaka miwili ya kifungo baada ya rufaa aliyokata kwenye mahakama kumpata hana makosa na kuwachiliwa huru.

“Mwanzo nilikuwa nimefungwa miaka mitano, nikapelekwa rumande. Niliona jinsi wananchi wa kawaida wanateseka, rufaa ikafanya nikapatikana sina makosa. Jela ni mahali pa kurekebisha na ndio maana nafahamu biblia,”alisema.

Anasema mpango wa kukamatwa ni kutokana na kutokuwepo na maelewana kati yake na Naibu wa Rais ambaye ni mpizani wake kutaka kufufua maovu aliyofanya miongo miwili iliyoipita.

“Mpango ulikuwa nikamatwe kila wakati. Nikafungwa siku tano wakati wa maandamano na kuhusishwa na dawa za kulevya. Mtu anayeenda mbinguni hawezi kufanya vitu kama hivyo” Aliongezea.

Alisisitiza kuwepo fununu za kufungua mambo ya kitambo ili kuwatatiza Wakenya wengine kwa tofauti za uongozi wa Mlima Kenya.

“Naona kampeni inayoendelezwa na Bw Rigathi akisema sisi hatuko, ndio sisi wa zamani hatuko. Kundi la Mungiki liliisha. Wale tuko ni watu wapya, damu mpya, Wakenya wapya na shughuli iliyopo ni kujenga Kenya iliyo na imani,” alielezea Bw Njenga.

Septemba 2023, aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga alikamatwa na watu wasiojulikana na kuachiliwa baada wa saa 24.

Wakati huo Wakili wake Ndegwa Njiru alilaani maafisa wa polisi kwa kumshika mteja wake.

  • Tags

You can share this post!

Maridhiano ‘yapiga hatua’ Azimio wakikubali kushiriki...

Disko Matanga sasa marufuku Kilifi kuzima kuchafuliwa kwa...

T L