Viongozi watangaza azma yao kuwania kiti cha ubunge Thika

Na LAWRENCE  ONGARO

KITI cha ubunge Thika kimewavutia wanasiasa kadha watakaojitosa uwanjani kupambana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Aliyekuwa mbunge hapo awali Bi Alice Ng’ang’a amejitosa ulingoni tena huku akitarajia kukigombania kiti hicho tena.

Naye Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha ugavana ambapo atapambana na Dkt James Nyoro ambaye ni gavana wa sasa.

Mwaniaji mwingine ambaye anatamani kujaribu bahati yake katika siasa ni afisa mkuu katika kampuni ya maji ya Thiwasco mjini Thika, Bw Juma Hemedi.

Kulingana na Bw Hemedi tayari wazee wa kiislamu wametoa baraka zao kwake  huku pia akitegemea kura za vijana.

Naye Bi Ng’ang’a,  aliyeshindwa na Bw Wainaina katika uchaguzi wa mwaka wa 2017, anasema amerejea kwa kishindo baada ya wafuasi wake wengi kumrai afanye hivyo. Katika uchaguzi huo Bi Ng’ang’a alizoa kura 50,115 huku mwenzake Bw Wainaina akipata kura 58,286.

Mwishoni mwa wiki Bi Ng’ang’a alizuru mji wa Thika na kupeana basari kwa wanafunzi wanaojiunga kwenye vyuo tofauti hivi karibuni.

Wakati wa hafla hiyo jumla ya Sh835,000 zilitolewa ili kuwanufaisha wanafunzi hao.

Kulingana na kiongozi huyo anasema angetaka kupewa nafasi nyingine na wananchi ili awafanyie kazi hasa kuhusu elimu na mayatima kazi aliyoenzi kufanya wakati wake.

Aliwarai wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua kura ili ifikapo wakati wa kupiga kura Agosti 2022, wawe wamejihami na silaha hiyo.

Alisema mivutano ya viongozi inayoshuhudiwa Mlima Kenya itatatuliwa hivi karibuni kwani “dakika ya mwisho jamii ya Mlima Kenya itazungumza kwa sauti moja.”

“Ninawasihi wananchi popote walipo wasiwe na uhasama miongoni mwao bali wawe watulivu na ikifika wakati wa kupiga kura wasichanganyikiwe na kuchagua viongozi wasio na maono,”  alifafanua kiongozi huyo.