• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Nigeria wazamisha Misri katika mechi ya Kundi D kwenye AFCON

Nigeria wazamisha Misri katika mechi ya Kundi D kwenye AFCON

Na MASHIRIKA

BAO la Kelechi Iheanacho lilisaidia Super Eagles ya Nigeria kupokeza Misri ambao ni mabingwa mara saba wa Kombe la Afrika (AFCON) kichapo cha 1-0 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi D kwenye kipute hicho mnamo Jumanne usiku nchini Cameroon.

Iheanacho ambaye ni fowadi matata wa Leicester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alifunga bao la pekee na la ushindi katika mchuano kati ya Nigeria na Misri katika dakika ya 30 mjini Garoua.

Nigeria walitamalaki mechi na wakazidia Misri maarifa katika takriban kila idara. Kipa El Shenawy wa Misri alifanya kazi ya ziada na kuwanyima Taiwo Awoniyi na Chidera Ejuke nafasi za kufungia Nigeria mabao zaidi.

Iheanacho aliridhisha zaidi katika safu ya mbele ya Nigeria – mabingwa mara tatu wa AFCON watakaokosa maarifa ya wavamizi matata Victor Osimhen, Emmanuel Dennis na Odion Ighalo kwenye makala ya 33 ya fainali za mwaka huu.

Nigeria walikuwa chini ya kocha mshikilizi Augustin Eguavoen huku mkufunzi wao mpya Jose Peseiro akiwa sehemu ya mashabiki. Peseiro aliteuliwa kujaza nafasi ya mkufunzi Gernot Rohr wiki nne kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa fainali za AFCON nchini Cameroon kupulizwa. Hatua hiyo ilichochewa na matokeo duni ya Nigeria kwenye kampeni za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo Disemba 2022.

Misri msukumo wa kushambulia na waliekeleza kombora moja pekee langoni mwa Nigeria chini ya kipindi cha dakika 70 licha ya kujivunia huduma za mvamizi mahiri wa Liverpool, Mohamed Salah. Ilikuwa hadi dakika za mwisho ambapo Salah alimshughulisha kipa Maduka Okoye wa Super Eagles.

Nigeria kwa sasa wanajiandaa kumenyana na Sudan katika mchuano ujao wa Kundi D mnamo Januari 15 huku Misri wakivaana na Guinea-Bissau siku hiyo.

Nigeria walitwaa ubingwa wa AFCON mara ya mwisho mnamo 2013 baada ya kupepeta Burkina Faso 1-0 nchini Afrika Kusini. Kwa upande wao, Misri ndio wanaojivunia mafanikio makubwa zaidi katika historia ya AFCON baada ya kuibuka mabingwa mara saba. Hata hivyo, hawajawahi kuonja ushindi wa taji hilo tangu 2010 walitandika Ghana 1-0 nchini Angola.

Mbali na Senegal, Nigeria na Misri, vikosi vingine vinavyopigiwa upatu wa kunyanyua ufalme wa AFCON mwaka huu ni Algeria, Ivory Coast, Morocco, Tunisia na wenyeji Cameroon.

Kwa kuwa Kundi D linajumuisha pia Guinea-Bissau na Sudan, Super Eagles ya Nigeria na Pharaohs ya Misri zinapigiwa upatu wa kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya AFCON nchini Misri.

Ndoto za Misri kujizolea taji la nane la AFCON mnamo 2019 ilisambaratishwa na Afrika Kusini waliowadengua katika hatua ya 16-bora kwa kichapo cha 1-0. Hata hivyo, wanajivunia kikosi thabiti mara hii chini ya kocha raia wa Ureno, Carlos Queiroz aliyetegemea zaidi maarifa ya Mohamed Elneny (Arsenal) na Mostafa Mohamed (Galatasaray) mbali na Salah.

Wanasoka waliotegemewa pakubwa na Nigeria kwa upande wao ni Samuel Chukwueze (Villarreal), Iheanacho na Wilfried Ndidi ambaye pia anatandazia Leicester City.

Hadi walipovaana kwenye makala ya AFCON mwaka huu nchini Cameroon, Nigeria na Misri walikuwa wamekutana mara 18 katika mashindano mbalimbali ya awali. Kati ya mechi hizo, Nigeria walikuwa wameshinda mara nane, Misri wakawika mara tano na wakaambulia sare mara tano.

Katika mechi 11 za AFCON ambazo sasa zimekutanisha vikosi hivyo, Nigeria wameshinda mara tano, Misri mara tatu na michuano mitano ikakamilika kwa sare.

Hadi waliposhuka dimbani nchini Cameroon, miamba hao walikutana mara ya mwisho katika mechi ya kirafiki mnamo 2019 ugani Stephen Keshi na Nigeria wakashinda 1-0.

Mbali na kukosa huduma za Abdullahi Shehu anayechezea Omonia nchini Cyprus, Nigeria walikuwa pia bila fowadi Osimhen wa Napoli aliyeugua Covid-19 na mvamizi mzoefu Ighalo ambaye waajiri wake Al Shabab nchini Saudi Arabia walikataa kumwachilia.

Misri nao walikosa maarifa ya wanasoka watatu – Mohamed Hamdy anayeuguza jeraha pamoja na Mohamed Abo Gabal na Ibrahim Adel walioambukizwa virusi vya corona wakiwa katika kambi ya mazoezi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Okutoyi aanza mazoezi nchini Australia baada ya vipimo...

Alice Ng’ang’a aongoza maandamano makali...

T L