• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mungu hutoa riziki kwa waja wake wanaoomba na kuitafuta kwa haki

Mungu hutoa riziki kwa waja wake wanaoomba na kuitafuta kwa haki

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Subuhaanahu Wata’ala, muumba wa kila kitu na kukiadiria muda wa kuishi hapa duniani.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam, Maswahaba wake watukufu na watangu wema hadi siku ya Kiyaama.Tunapoendelea na mawaidha yetu ya kila Ijumaa, ni vyema tuombeane kheri na kumwomba Allah atulinde kutokana na janga hili la corona linalozidi kutetemesha ulimwengu mzima.

Huu ni mtihani ambapo Allah anaziweka imani zetu kwenye mizani, ama tukufuru au tumshukuru yeye. Muhimu ni kuzingatia maelekezo yanayotolewa na washika dau katika sekta ya afya ili kuepuka maambukizi yake.

Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa ubora zaidi na kumjaalia neema za kila aina katika uhai wa maisha yake. Katika Quran Tukufu pia imebainishwa kwamba, Mwenyezi Mungu ametujaalia neema nyingi zisizokuwa na kipimo.

Riziki ni neema inayotoka kwa Mwenyezi Mungu anayowajaalia viumbe wote hapa duniani. Kila kiumbe hujaaliwa riziki na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya uhai wake.Mojawapo ya majina ya sifa za Mwenyezi Mungu ni ‘Ar-Razzak’.

Hii ina maana kwamba, yeye pekee ndiye mtoaji riziki kwa viumbe. Mwenyezi Mungu anatoa riziki kwa viumbe wote na wala sio kwa Waislamu pekee. Wanadamu wanatakiwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila neema kubwa na ndogo anazowajaalia kwa ajili ya maisha yao.

Kuna aya mbalimbali zinazozungumzia neema ya riziki inayotolewa na Mwenyezi Mungu pekee.Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja wake wanaoomba riziki na kutafuta kwa njia inayofaa. Katika mojawapo ya hadithi za Mtume Muhammad, pia tunahimizwa kutokata tamaa wala kupoteza matumaini maishani tunapokosa kitu tunachokitafuta kwa kuwa Mwenyezi Mungu pekee ndiye mtoaji na anayejuwa zaidi.

Wanadamu huzaliwa na kuja duniani bila chochote lakini baadaye Mwenyezi Mungu anamruzuku na kumneemesha kwa hali na mali.Waja wema wanaomwamini Mwenyezi Mungu kikamilifu hawawezi kuwa na hofu wala wasiwasi kuhusu suala la riziki.

Mtoto anapokuwa tumboni mwa mamake au viumbe wadogo wanaoishi chini ya bahari hujaaliwa riziki na Mwenyezi Mungu pasi na kuihangaikia. Lakini viumbe wengine wote wanapaswa kuhangaika au kujishughulisha na utafutaji riziki ili Mwenyezi Mungu aweze kuwajaalia.

Wanapaswa kuitafuta riziki kwa njia ya halali na isiyokiuka kanuni au sheria za dini ya Kiislamu zilizoamrishwa na Mwenyezi Mungu.Riziki ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu. Yeye pekee ndiye anayejaalia na wala haiwezi kutolewa na kiumbe mwingine yeyote.

Kadri mtu anavyozidi kujituma kuisaka riziki, hivyo ndivyo riziki yake inavyozidi kumtafuta. Katika maisha ya hapa duniani, kuna mtihani mkubwa tunaokumbana nao kuhusu suala la riziki na maajaliwa. Wapo wanaojaaliwa riziki nyingi na wengine riziki kidogo.

Haya yote ni mitihani tuliyowekewa na Mwenyezi Mungu mwenyewe anayezijua zaidi.Aya nyingi za Quran tukufu pamoja na hadithi za Mtume Muhammad zinasisitiza umuhimu wa kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa neema tunazojaaliwa.

Wanadamu wanatakiwa kuridhishwa na neema ambazo ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtume Muhammad pia ametufunza dua tunayopaswa kuisoma kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Dua yenyewe ni hii;“Mola wangu, nisamehe madhambi yangu, unizidishie riziki yangu na kuitia baraka ndani yake!”Kila neema inayotolewa na Mwenyezi Mungu basi inapaswa kutumiwa vyema na kutolewa shukrani kubwa kwa mtoaji.

Suala la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni msingi muhimu wa mafunzo ya dini ya Kiislamu. Muumini wa kweli aliyekuwa na imani kamilifu hawezi kumtegemea mja mwenzie au kiumbe kingine chochote kwa ajili ya kumpa riziki.

Badala yake, tegemeo lake kubwa lipo kwa Mwenyezi Mungu pekee ambaye ndiye mtoaji na anayejaalia.Muumini wa kweli pia hawezi kumuonea mwenzie wivu au kumuwekea chuki kwa riziki aliyojaaliwa.

Hii ni kwa sababu anaamini kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye mtoaji na yeye pekee ndiye anayegawa riziki kwa jinsi anavvyotaka. Mtume Muhammad pia anatueleza katika hadithi yake kwamba, kila mwanadamu hujaaliwa riziki kwa kiwango maalum anachostahiki.

Hivyo basi tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila hali pasi na kuweka chuki, husuda au wivu wa aina yoyote.

  • Tags

You can share this post!

euro hiyo…

Mashabiki Nakuru kuona Safari Rally angani kwa ndege