• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
2022: Wanawake watakaowania nyadhifa kufadhiliwa

2022: Wanawake watakaowania nyadhifa kufadhiliwa

Na BERNARDINE MUTANU

Wanawake wanaoazimia kuwania nyadhifa za kisiasa 2022 watanufaika baada ya shirika lisilo la serikali kuzindua amana ya kuwafadhili wakati wa kampeni.

Amana hiyo haitawafaa wanawake wanaowania nafasi za kisiasa pekee, lakini wote wanaotafuta nafasi za uongozi katika viwango vyote nchini.

Hazina hiyo ilizinduliwa rasmi na Waziri wa Huduma za Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Bi Margaret Kobia kwa lengo la kukuza demokrasia nchini.

Wakati wa mkutano na wanahabari Jumatano asubuhi Jijini Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa Echo Trust, ambayo awali ilikuwa ni Kenya Women Holding Dkt Jennifer Riria alisema uzinduzi wa amana hiyo, Democracy Trust Fund (DTF) ni kuwasaidia wanawake wengi zaidi kukwea nyadhifa za uongozi.

“Ni wakati wa kuwa na magavana na maseneta zaidi nchini. Tunataka kuweka wazi uongozi wa wanawake nchini,” alisema Dkt Riria.

Kulingana naye, kupitia kwa amana hiyo, wanawake watakuwa na uwezo wa kufadhili kampeni zao ifikapo wakati wa kutafuta nyadhifa.

Lakini wanatakiwa kuweka pesa katika hazina hiyo pole pole mpaka watakapohitaji kuitumia “kulingana na nyadhifa za uongozi” wanazotafuta, alisema mkurugenzi huyo.

Pesa hizo zitapokelewa na benki simamizi na kuwekezwa kwa lengo la kukuza zaidi kiwango cha pesa walizohifadhi, na watakazochukua wakati wa kampeni.

“Hakuna kiwango cha mwisho ambacho mwanamke anaweza kuhifadhi. Utakuwa utaratibu wazi kwa sababu tayari tumeweka mfumo dhabiti,” alisema Dkt Riria.

Kulingana naye, shirika hilo limetenga taifa kwa maeneo 12 ambako maafisa wake watazuru na kuhamasisha wanawake kuhusiana na hazina hiyo.

Wanawake wote wanaotafuta nyadhifa za uongozi na walio na miaka 18 na zaidi watapokea mafunzo chini ya mpango kwa lengo la kuimarika kiuongozi na kujua jinsi ya kujifadhili zaidi wakati wa kampeni bila kujali chama au mwegemeo wa kisiasa, alisema.

“Tunataka kunoa wanawake ili kuhakikisha kuwa kuna uongozi wa pamoja na wa haki katika jamii,” alisema Dkt Riria.

Shirika hilo linashirikiana na mashirika mengine kama vile Wizara ya Huduma za Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia, Global Fund for Women na UN Women, ili kuhakikisha kuwa mpango huo umefaulu.

You can share this post!

DHULUMA KWA WANAHABARI: Muthoki Mumo alivyoteswa na polisi...

AKILIMALI: Mwalimu anavyotumia teknolojia kuvuna hela...

adminleo