• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
PUFYA: Sumgong aongezwa marufuku hadi 2025 kwa kutoa ushahidi wa uongo

PUFYA: Sumgong aongezwa marufuku hadi 2025 kwa kutoa ushahidi wa uongo

Na GEOFFREY ANENE

JEMIMAH Sumgong ameongezwa adhabu ya kutumia dawa ya kusisimua misuli ya EPO kutoka miaka minne hadi minane baada ya jopo huru la nidhamu katika Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kutupilia mbali madai yake kwamba dawa hizo ziliingia mwilini mwake baada ya “daktari bandia” kumdunga sindano katika hospitali moja madkatari wakiwa kwenye mgomo.

Adhabu hii ya kipekee ilifanywa baada ya jopo hilo kuamua kuna “ushahidi wa kutosha” kwamba Sumgong pia alikuwa ametumia stakabadhi ghushi za matibabu na kudanganya kuhusu mahali alikokuwa baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa ya aina ya EPO mwaka 2017, ambayo ilimfanya apigwe marufuku miaka minne mwaka 2017.

Marufuku hiyo, ambayo ilianza Aprili 3, 2017, imeongezwa na IAAF Ijumaa baada ya jopo hilo likiongozwa na Michael Beloff QC, kuamua kwamba mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 34 alikuwa amevunja sheria za kukabiliana na matumizi ya pufya kwa mara ya pili kwa “kuvuruga shughuli za kudhibiti matumizi ya pufya”.

Kwa sasabu ya mabadiliko katika sheria za Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli, Mkenya huyu aliweza kuadhibiwa kwa kuongezwa marufuku yake maradufu.

Hukumu hii inamaanisha kwamba Sumgong, ambaye ni Mkenya wa kwanza kabisa mwanamke kushinda marathon katika Michezo ya Olimpiki aliponyakua ubingwa wa mwaka 2016 nchini Brazil, atatumikia marufuku hadi Aprili 3, 2025.

Habari hizi zimepokelewa vyema na mkuu wa kitengo cha maadili cha riadha (AIU), ambaye anasema ni pigo kubwa kwa watumiaji wa dawa za kusisimua misuli nchini Kenya.

“Tunatumai hii itakuwa funzo kwa wahalifu wa dawa zilizopigwa marufuku katika michezo kwamba AIU ina uwezo wa kufanya uchunguzi wake na hairuhusu ushahidi wa uongo katika kesi za matumizi ya dawa za kusisimua misuli,” alisema.

“Tungependa pia kushukuru kazi ya Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya la Kenya (ADAK) katika kufuatilia kesi hii. Wao ni washirika muhimu katika vita dhidi ya matumizi ya pufya nchini Kenya.”

You can share this post!

Presha kwa Shujaa katika michuano ya Hamilton Sevens

KJMA yakemea wanaokejeli Idara ya Mahakama

adminleo