• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya kina kuhusu dhana ya Isimu

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya kina kuhusu dhana ya Isimu

Na MARY WANGARI

KATIKA matini zilizotangulia, tulilinganisha na kulinganua jinsi dhana za isimu zinavyohusiana na kutofautiana kwa jumla.

Hii leo, tutachunguza kwa kina dhana ya isimu kwa jumla kwa kuangazia vipengele anuwai jinsi ifuatavyo:

Isimu

Dhana ya isimu imefasiliwa na wataalam mbalimbali ambao wametoa fasili zao kuihusu jinsi ifuatavyo:-

Kwa mujibu wa Massamba  (2004), isimu ni taaluma ya ufafanuzi, uchambuzi na uchanganuzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi.

Kwa upande wake Hartman (1972), anaeleza isimu kama eneo mahsusi la mtaala ambalo lengo lake huwa ni kuichunguza lugha.

Wanaisimu huzichunguza lugha kama nyenzo muhimu za kuwezesha mawasiliano ya mwanadamu.

Naye Besha (1994), anadadavua kwamba isimu ni taaluma ambayo huchunguza na kuweka bayana kanuni ambazo ndizo msingi wa kila lugha.

Hivyo basi, kundi hili la wataalam linafasili isimu kuwa ni taaluma inayohusika na ufafanuzi, uchambuzi na uchanganuzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi. Mbinu hizo zinaweza kuhusisha michakato ifuatayo:

  1. uchunguzi uliodhibitiwa
  2. uundaji wa mabunio
  3. uchanganuzi
  4. ujumlishi
  5. utabiri
  6. majaribio na uthibitishaji
  7. urekebishaji au ukataaji wa mabunio

Jamii kwa upande wake inaweza kuelezwa kama  mkusanyiko wa watu wanaoishi kwa pamoja katika eneo moja la kijiografia wakiunganishwa na historia yao na wakitambuliwa kwa utamaduni wao, lugha, mila na itikadi zao na kadhalika.

Msanjilla na wenzake (2011) wanasema kwamba isimujamii ni taaluma inayoshughulika na matumizi ya lugha katika jamii.

Naye King’ei (2010), anasema isimujamii ni taaluma inayo eleza uhusiano wa karibu ulio kati ya matumizi ya lugha na maisha ya jamii.

Isitoshe, anazidi kufafanua kwamba lugha ni zao la jamii na ni kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii.

Aidha, lugha hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya kuhifadhi amali na utamaduni wake na hususan kama chombo maalum cha kuwezesha wanajamii kuwasiliana.

Isimujamii hueleza na kufafanua mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha au ukipenda unaweza kueleza jamii kama kitovu cha lugha.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili ni Teacher Training Colleges in Tanzania”.                  Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991). “English versus Kiswahili in Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studies Ghent.

You can share this post!

Viongozi kadha wasema raia wanathubutu ‘kuwaua ndugu...

Christine Kathure Kendi: Haijalishi umetoka wapi

adminleo