• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
NDIVYO SIVYO: Hii hapa nususi ya usahihi wa baadhi ya maneno ambayo ni sehemu ya msamiati wa jamaa au ukoo

NDIVYO SIVYO: Hii hapa nususi ya usahihi wa baadhi ya maneno ambayo ni sehemu ya msamiati wa jamaa au ukoo

Na ENOCK NYARIKI

IJAPOKUWA lugha za Kiafrika zina utajiri wa msamiati unaotumiwa kuwaitia jamaa wa mume au mke, si watu wengi wanaweza kuufasiri msamiati huu kwa lugha ya Kiswahili.

Baadhi yao, kwa mfano, hulitumia neno “shemeji” kwa maana ya wakwe na jamaa wengine wa upande wa mke au mume.

Kosa hili linatokana na fasiri potovu ya msamiati wenyewe.

Hebu sasa tuwaangazie “jamaa wengine wa upande wa mume au mke” tuliowatanguliza katika makala haya.

Toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu linaeleza kuwa neno muamu ni kisawe cha shemeji. Waama, hiyo ni njia ya jumla mno ya kulifasili neno hilo na huenda mtu ambaye haufahamu msamiati shemeji asilielewe neno muamu. Tutayafafanua madai haya baadaye.

Wifi ni jina la heshima la kifamilia waitanalo mke na ndugu wa kike wa mume. Maneno ‘ndugu wa kike wa mume’ ni muhimu sana katika kulipa neno hili fasili yake.

Wifi anaweza pia kuelezwa kuwa ni dada ya mume au ni shemeji wa jinsia ya kike katika upande wa mume.

Fasili ya mwisho ya neno hili inaweza kumkanganya mtu ambaye hafahamu maana ya neno shemeji.

Kwa hivyo, ni muhimu tulifafanue neno hilo.

Shemeji ni ndugu wa mkeo au mumeo au ni mume au mke wa ndugu yako.

Madai ya baadhi ya wanasarufi kuwa muamu ni ndugu wa kiume wa mume si kweli.

Hakika hili ni neno la jumla linalotumiwa kuwarejelea ndugu wa mke au mume wa mtu.

Kwa hivyo, muamu anaweza kuwa ndugu wa kiume au wa kike wa mume au mke wa mtu. Katika Kimaragoli, jina hilo hutamkwa kama “mlamwa” likiwa na maana tuliyokwisha kuitaja.

Wakwe nalo ni jina la jumla linalotumiwa kuwaitia bavyaa, mavyaa, baba mkwe na mama mkwe.

Mavyaa na bavyaa ni msamiati ambao aghalabu hutumiwa kuwarejelea wakwe wa upande wa mume ilhali baba mkwe na mama mkwe hutumiwa kuwarejelea wacheja wa kuukeni.

Jina jingine linalokaribiana sana na mkwe ni kivyere. Kivyere ni jina la heshima wanaloitana wakwe wa kuumeni na kuukeni.

Fasiri yake katika Kimaragoli ni “basangi” lenye maana ya ‘niliyeshirikiana naye’ katika kuzileta familia mbili pamoja.

Alhasili, neno shemeji halipaswi kutumiwa kuwarejelea wakwe au wacheja hata pale ambapo lengo la mzungumzaji ni kuzungumzia jamaa wengine wa mke au mume.

Shemeji ni ndugu wa mke au mume ama ni mume au mke wa ndugu yako. Mkwe naye ni mzazi wa mume au mke.

You can share this post!

Kigogo: Tamthilia inayotabiri kuporomoka kwa viongozi...

USWAHILINI: Kujisitiri mwanamke wa Uswahili kiini si dini,...

adminleo