• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Shule za kibinafsi kimbilio licha ya gharama

Shule za kibinafsi kimbilio licha ya gharama

Na KARIUKI WAIHENYA

Wakenya wengi wanapendelea shule za kibinafsi licha ya serikali kutoa elimu ya msingi bila malipo na kupunguza karo katika shule za sekondari za umma.

Watu wa mapato ya wastani huwa wanapuuza shule za umma na kuwapeleka watoto katika shule wanazolipa kati ya Sh50,000 na Sh800,000 kwa muhula mmoja.

Baadhi yao huchukua mikopo au kutumia akiba yao kulipa karo katika shule za kibinafsi.

Kulingana na takwimu kutoka Wizara ya Elimu, idadi ya shule za kibinafsi imeongezeka zaidi ya maradufu katika muda wa miaka minne iliyopita kutoka 7,742 mwaka wa 2014 hadi 16,594 mwaka wa 2019.

Kwa upande mwingine, shule za msingi za umma zimeongezeka kwa 1,728 kutoka 21,718 mwaka wa 2014 hadi 23,446 mwaka huu.

Hali ni kama hiyo kwa shule za sekondari, ambako shule za kibinafsi zimeongezeka mara nne kutoka 1,048 mwaka wa 2014 hadi 4,310 mwaka wa 2019.

Shule za sekondari za umma zimeongezeka kwa 1,731 kutoka 7,686 mwaka wa 2014 hadi 9,417 mwaka huu.

Dkt Geofffrey Wango, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi alisema wazazi wanaosomeshea watoto wao katika shule za kibinafsi wanalenga elimu bora.

“Shule za kibinafsi zina vifaa bora, hazina msongamano na zina utaratibu mzuri na muundo mwema,” alisema.

Alilaumu uhaba wa walimu katika shule za umma na ukosefu wa motisha na ukosefu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi kwa ongezeko la shule za bei ghali.

Juhudi za serikali za kutoa masomo ya bure katika shule za msingi zimefanya idadi ya wanafunzi katika shule za umma kuongezeka.

Mwaka wa 2003, idadi ya wanafunzi waliokuwa katika shule za msingi ilikuwa ni milioni 5.3. Lakini mwaka wa 2019, idadi ya watoto walioko katika shule za msingi ni milioni 8.8.

Katika shule za sekondari, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 800,000 hadi 2.8 milioni.

You can share this post!

Mvua sasa kuchelewa kufuatia kimbunga Idai

Mudavadi adai mabwawa ni njama ya uporaji

adminleo