• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
‘Tangatanga’ wamtafuna Matiang’i

‘Tangatanga’ wamtafuna Matiang’i

ANITA CHEPKOECH na BENSON AMADALA

VIONGOZI walio katika kambi ya Naibu wa Rais, maarufu Tanga Tanga, wamemgeuzia Waziri wa Usalama Fred Matiang’i hasira zao kwa kusema ‘amehatarisha’ usalama wa Dkt William Ruto.

Viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Belgut Nelson Koech, seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale na viongozi wa vijana kutoka eneo la North Rift pia wameshutumu Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho kwa kukosa kumhakikishia usalama Dkt Ruto alipozuru eneo la Tetu, Kaunti ya Nyeri, wiki iliyopita.

Viongozi hao walisema hiyo ni njama inayolenga kusambaratisha azma ya Dkt Ruto kushinda urais 2022.

Jumamosi, Bw Kibicho alishutumu afisi ya Dkt Ruto kwa kukosa kuripoti katika Wizara ya Usalama kuhusiana na ratiba ya ziara zake nchini, ili maafisa wakuu wa usalama watumwe katika hafla zake.

Mbunge wa Belgut hata hivyo, alisema maelezo hayo ya Bw Kibicho hayana mashiko.

“Naibu wa Rais ni mtumishi wa serikali na afisi yake imekuwa ikieleza Wizara ya Usalama kuhusiana na ziara za Dkt Ruto tangu 2013. Siamini kwamba afisi yake imeacha kufahamisha wizara kuhusu ziara zake kwa sababu baadhi ya wafanyakazi katika afisi hiyo wanalipwa kufanya hivyo,” akasema Bw Koech.

Mbunge huyo aliapa kuwasilisha hoja hiyo bungeni, huku akidai kuwa hatua ya maafisa wa ngazi za juu kukosa katika hafla ya Dkt Ruto ni njama inayodhamiria kummaliza kisiasa kabla ya 2022.

Dkt Khalwale aliyekuwa akizungumza kijijini Lubao, Kaunti ya Kakamega jana, alisema viongozi wa ngazi za juu serikalini wameanza mpango wa kumhangaisha Dkt Ruto kwa lengo la kumshinikiza kujiondoa katika kinyang’anyiro cha urais.

Alimtaka Dkt Matiang’i akome kujiingiza katika siasa za kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

“Nawataka Matiang’i na Kibicho wanisikilize kwa makini. Wanafaa kukoma kutumia nyadhifa zao kujihusisha na siasa za urithi za 2022. Wanafaa kufahamu kuwa watawajibika endapo chochote kitamfanyikia Naibu wa Rais,” akasema Dkt Khalwale aliyekuwa akihutubia waombolezaji katika eneo la Lubao.

Vijana kutoka maeneo ya North Rift wakiongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Vijana kutoka Kerio, Bw Joel Kimaiyo walimtaka Dkt Matiang’i na Bw Kibicho kumheshimu Naibu wa Rais.

Vijana hao waliwataka wakuu hao wa Wizara ya Usalama wakome ‘kucheza’ na usalama wa Naibu wa Rais.

“Naibu wa Rais ana haki ya kikatiba kupewa ulinzi. Hiyo ni haki ya kikatiba na wala si msaada,” akasema Bw Kimaiyo.

Bw Kibicho, Jumamosi, alitetea wizara hiyo huku akipuuzilia mbali madai kwamba Naibu wa Rais amepokonywa walinzi.

“Kibicho anafaa kukoma kuwapotosha Wakenya. Alitwambia kwamba afisi ya Naibu wa Rais haikufahamisha wizara kuhusu wizara yake katika eneo la Tetu ilhali Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Tetu, Bw Odhiambo alisema kuwa alifahamu kuhusu ziara ya Dkt Ruto siku tatu kabla,” akasema Bw Kimaiyo.

Bw Koech alisema kuna uwezekano kwamba machifu na maafisa wa ngazi za juu wa usalama wa kaunti hiyo waliagizwa na wizara kutohudhuria hafla ya Dkt Ruto.

Dkt Khalwale alidai kwamba Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanatumia handisheki kummaliza kisiasa Dkt Ruto kabla ya uchaguzi wa 2022.

You can share this post!

Neno-siri linalotumika zaidi duniani ni...

Gor Mahia Youth na Tandaza FC moto wa daraja ya pili

adminleo