• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
MAKALA MAALUM: Wageukia magari ya serikali kusafirisha miti ili wasikamatwe

MAKALA MAALUM: Wageukia magari ya serikali kusafirisha miti ili wasikamatwe

Na BERNADINE MUTANU

TANGU kupigwa marufuku kwa ukataji wa miti na uchomaji makaa, wafamyibiashara wa bidhaa hizo wamelazimika kuja na mbinu mpya.

Ripoti za majuzi, zinaonyesha kuwa watu hao sasa wanatumia magari ya serikali bila kushukiwa ingawa baadhi yao wamekamatwa.

“Biashara ya bidhaa hizo imenoga sana na ndio maana watu wametafuta mbinu za kusafirisha bidhaa hizo,” alisema afisa ambaye hakutaka jina lake kuchapishwa kwa sababu ya umuhimu wa suala hilo.

Kutokana na agizo la Naibu wa Rais William Ruto mnamo Februari, marufuku ya ukataji miti na biashara ya bidhaa za misitu kote nchini itaendelea kwa muda wa miezi mitatu.

Tangazo lake lilitokana na upungufu wa maji mitoni na ukame mkubwa ulioshuhudiwa nchini, kabla ya mvua ya masika kuanza kunyesha.
Kutokana na operesheni kali iliyoanzishwa, imewabidi wafanyibiashara kufanya biashara hiyo kwa njia ya siri kama ilivyobainika.

Gari la polisi liliponaswa eneo la Kapenguria likisafirisha mbao. Picha/ Oscar Kakai

Wiki iliyopita, malori matatu ya jela yalikamatwa yakibeba mbao katika eneo la Eldama Ravine. Kisa hicho kilitokea siku moja tu baada ya lori la polisi wa utawala (AP) kukamatwa eneo la Chepkworniswo.

Mnamo Machi 30, lori la askari wa utawala lilikamatwa katika eneo la Marereni, Kaunti Ndogo ya Magarini, Kaunti ya Kilifi likiwa na magunia 120 ya makaa.

Hata hivyo, afisa wa KFS wa ngazi ya chini akizungumza na Taifa Leo alitetea magari ya serikali kwa kusema kati ya magari 63 yaliyokamatwa tangu operesheni kuanzishwa, ni manne tu ya serikali yaliyokamatwa.

“Sio vyema kusema magari ya serikali ndiyo yanasafirisha bidhaa za msituni kwa sababu kati ya magari 63 yaliyokamatwa, ni manne pekee ambayo ni ya serikali,” alisema afisa huyo.

Aidha, wauzaji wa bidhaa za misitu wanasafirisha bidhaa hizo usiku ili kuepuka makachero wa Huduma ya Misitu (KFS) na maafisa wa polisi.

Kwa mfano, mwanzoni mwa Machi, dereva mmoja alikamatwa na kushtakiwa katika Mahakama ya Embu kwa kusafirisha magogo bila idhini.

Malori 3 ya jela yaliyokamatwa yakisafirisha mbao Eldama Ravine. Picha/Ayub Muiyoro

Malori ya kontena

Pia, malori yanayobeba kontena yanakisiwa kuingilia biashara hiyo ambayo kwa sasa imeharamishwa.

Wiki iliyopita, lori moja lilipigwa picha eneo la South B, katika Barabara ya Nairobi kuelekea Mombasa likimwaga bidhaa hiyo inayotumiwa na asilimia kubwa zaidi ya wakazi wa Nairobi.

Hii ni kutokana na kuwa malori ya kontena hayasimamishwi barabarani na polisi na pia ukweli kwamba huwa yamefungwa kabisa kutoka depo au chanzo cha bidhaa.

Pia, magari ya abiria na yale ya kibinafsi yanatumiwa kusafirisha makaa maeneo mbali mbali nchini.

“Hii ni biashara ambayo ina faida nyingi na ndio maana magari ya serikali yanatumiwa kuiendeleza,” alisema mdokezi mmoja.

Kufikia mwishoni mwa juma jana, magunia 300 ya makaa yalikuwa yamekamatwa eneo la Pwani tangu kuanzishwa kwa operesheni hiyo.

Licha ya hatua kali, bado biashara hiyo imeonekana kuendelea katika baadhi ya maeneo Kilifi na Tana River ambako malori saba, mabasi matatu na pikipiki sita yalikamatwa yakisafirisha aidha makaa au mbao.

Mabasi hayo yalipatikana na magunia 105. Polisi walidokezewa baadhi ya visa hivyo na umma.

 

 

You can share this post!

Mganda Chesang’ avunja utawala wa Kenya mita 10,000

Pasta ashangaza kuomba waumini idhini afurushe mkewe

adminleo