• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Matiang’i adai wakosoaji wake wamekerwa kukosa tenda

Matiang’i adai wakosoaji wake wamekerwa kukosa tenda

PETER MBURU na IBRAHIM ORUKO

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiangí anasema hatishwi na ‘kelele za chura’ na kwamba, wanaomsingizia makosa wana hasira kwa kukosa zabuni katika wizara yake.

Alisema kuna baadhi ya watu ambao wanataka kutumia hila kupata zabuni katika idara ya usalama, lakini akaonya kuwa hatasita kutenda haki kwani ndiyo kazi aliyopewa.

Kulingana na Dkt Matiangi, watu wanaomchafulia jina wanataka kumnyamazisha kwa kuwa wamekosa zabuni katika sekta hiyo, akisema ni hao wanaoharibu taifa kwa kulinyima maendeleo.

“Hatuwezi kukubali kufa sote katika meli tukitorokea Ulaya kwa kuwa mtu fulani ameharibu taifa letu. Kwa kuwa anataka zabuni katika sekta ya usalama. Eti anataka anihangaishe nikubali hila zake. Hilo halitafanyika,” akasema Dkt Matiangi.

Waziri huyo alisema aliamua kufanya haki na ukweli alipokubali kazi hiyo, akisisitiza kuwa hatasikiza kelele za watu walio na nia zisizo na manufaa kwa taifa.

Alisisitiza usemi wake wa mbeleni kuwa hakuajiriwa ili kuwa maarufu, ila kuleta maendeleo na mageuzi ya umuhimu kwa taifa.

Ingawa hakufafanua aliokuwa akiwarejelea Jumatano, kamati ya Bunge la Seneti iliyochunguza kuuzwa kwa uwanja wa shule ya Ruaraka, ilipendekeza waziri huyo achunguzwe, na akipatikana na hatia afunguliwe mashtaka.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay, Bw Moses Kajwang’ inapendekeza kuwa waziri huyo awajibike dhidi ya kufujwa kwa Sh1.5 bilioni za mlipa ushuru.

Alikuwa akizungumza jijini Nairobi katika hafla ya kuaga makamishna wa Tume ya Uwiano na Maridhiano nchini (NCIC) ambao muda wao wa kuhudumu ulimalizika jana.

You can share this post!

NENDENI SALAMA: Misa ya kuaga wanafunzi 10 yaandaliwa

Waislamu washukuru Saudia kudhamini mahujaji, kupanua...

adminleo