• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Joho achemsha Wiper kuhusu kiapo

Joho achemsha Wiper kuhusu kiapo

BONFACE MWANIKI na BENSON MATHEKA

Kwa ufupi:

  • Bw Joho amtaja Bw Musyoka na vinara wengine wawili wa NASA kama waoga kwa kutohudhuria kiapo cha Bw Raila Odinga
  • Bila kutaja majina, Bw Musyoka awalaumu wanasiasa wa ODM kwa kumuita mwoga
  • Bw Wambua asema matamshi ya Bw Joho ni madharau kwa Bw Musyoka na vinara wengine wa NASA
  • Wiper yasema haitakubali wabunge, magavana na hata madiwani wa ODM kuwatusi vinara wa NASA

NYUFA katika muungano wa NASA zinaendelea kupanuka huku wanasiasa wa chama cha Wiper wakimshutumu Gavana wa Mombasa Hassan Joho na chama cha ODM kwa kile wanachosema ni dharau dhidi ya kiongozi wa chama chao, Bw Stephen Kalonzo Musyoka.

Seneta wa Kitui, Enoch Wambua (Wiper), alimlaumu Bw Joho na viongozi wa ODM akisema kwamba wanachama wa Wiper hawatakubali mtu yeyote kumdharau kiongozi wao.

Akihutubia mkutano wa baraza kuu la ODM jijini Nairobi Ijumaa iliyopita, Bw Joho alimtaja Bw Musyoka na vinara wengine wawili wa NASA, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kama waoga kwa kutohudhuria kiapo cha Bw Raila Odinga.

Bw Musyoka na Bw Mudavadi walihudhuria mkutano huo kwa mwaliko wa kiongozi wa chama hicho Raila Odinga.

Akihutubia wajumbe katika mkutano huo, Bw Musyoka aliwataka wanasiasa wa vyama tanzu vya NASA kuheshimu vinara wote. Bila kutaja majina, aliwalaumu wanasiasa wa ODM kwa kumuita mwoga.

 

Madharau

Bw Wambua alisema matamshi ya Bw Joho ni madharau kwa Bw Musyoka na vinara wengine wa NASA ambao hawakuhudhuria mkutano wa kumuapisha Bw Odinga kuwa “rais wa wananchi” katika bustani ya Uhuru Park mnamo Januari 30.

“Kama chama, hatutakubali matusi kutoka kwa viongozi wengine waliochaguliwa chini ya muungano wa NASA. Kuwatusi vinara wetu kunafaa kuwa kitu cha mwisho kutoka kwa viongozi. Mimi mwenyewe siwezi kuthubutu kufanya hivyo,” alisema Bw Wambua.

Aliambia chama cha ODM kwamba Wiper ina mbinu nyingi za kutumia iwapo wanasiasa wake wataendelea kumdharau Bw Musyoka.

“Kama wenzetu katika ODM wanafikiri tumekwama NASA, wajue Wiper ina mbinu nyingi na tuko tayari kufuata mojawapo tukilazimishwa kufanya hivyo. Wanafaa kuwa waangalifu sana,” alionya Bw Wambua.

 

‘Hatutakubali matusi’

“Hatuwezi kukubali hali ambapo wabunge, magavana na hata madiwani wana ujasiri wa kuwatusi vinara wa muungano wetu,” alisema Bw Wambua.

Seneta huyo alisema vyama tanzu katika Muungano wa NASA ni sawa na vinafaa kuheshimiana.

Akiongea eneo la Mwingi, Bw Wambua alisema kuwa Wiper inaendelea kuweka mikakati ya kujiimarisha ili kuhakikisha Bw Musyoka anashinda urais mwaka wa 2022.

“Tutatangaza mikakati mipya ili kuhakikisha ifikapo 2022, kiongozi wa chama chetu Kalonzo Musyoka atakuwa rais wa Kenya kwa manufaa ya wote,” alisema.

Bw Wambua alisema Wiper kinajiandaa kusajili wanachama wengi kote nchini kama njia moja ya kukiimarisha.

Wiper pia kimekuwa kikilaumu ODM kwa kutwaa nafasi za kamati za bunge ambazo zingegawiwa vyama tanzu.

 

You can share this post!

JAMVI: Sababu ya Uhuruto kufurahia ukaidi wa Raila kwa...

Wazee sasa wamgeukia Mungu amalize njaa

adminleo