TAHARIRI: Huu uwe mwaka wa kujirekebisha

KITENGO CHA UHARIRI

MWAKA wa 2020 ulikuja na changamoto za aina yake, nyingi ambazo hazijawahi kushuhudiwa na wengi nchini na hata ulimwenguni kote.

Changamoto hizo ambazo nyingi zililetwa na janga la virusi vya corona zilifanya hali ya maisha iwe ngumu kwa idadi kubwa ya wananchi.

Hata hivyo, si siri kwamba Wakenya wengi walikuwa tayari wanakabiliwa na hali ngumu ya kimaisha hata kabla janga la corona kuanza kusambaa ulimwenguni.

Katika miaka iliyotangulia, changamoto kama vile ukosefu wa ajira na mandhari duni ya kufanyia biashara kwa hali inayoleta faida zilikuwa tayari zinateza wengi.

Wakati huo, changamoto hizo zililaumiwa sana kwa ufisadi ambao hushuhudiwa serikali kuu na za kaunti.

Kile ambacho janga la corona lilifanya, ni kuongeza taabu juu ya balaa ambazo zilikuwa tayari zipo humu nchini.

Tunapoanza mwaka mpya wa 2021, taswira inayoonekana hadharani ni kuwa hakuna matumaini ya kutosha kwamba hali itaanza kuwa bora hivi karibuni.

Serikali ilishindwa kutenda mambo ambayo yangewaletea wananchi matumaini kwamba watasaidiwa kutatua changamoto ambazo wanapitia.

Hii ni kutokana na kuwa, hata wakati ilipotarajiwa maafisa serikalini wangelikuwa na utu, bado sakata za ufisadi zilitokea katika juhudi za kupambana na janga la corona ambalo lilisababisha maafa tele na hasara za kiuchumi na kijamii katika nchi hii.

Raia wengi wa kawaida hujitolea mhanga kila siku kujitafutia riziki kwa njia yoyote ile ya haki, huku wakitozwa ushuru tele kwa matarajio ya kupokea huduma bora ambazo zitasaidia kuinua maisha yao.

Kwa msingi huu, itakuwa ni unyama kama serikali itaingia mwaka wa 2021 bila kuweka kando mienendo isiyokuwa na manufaa kwa umma.

Mwaka huu tunaoingia unatarajiwa kuwa na shughuli tele za kisiasa kwani umekaribia mwaka wa uchaguzi mkuu 2022, na vile vile shughuli za kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Ni matumaini yetu kuwa viongozi wote wanaotegemewa kubuni na kutekeleza sera muhimu za kitaifa watakumbuka majukumu yao ya kutumikia taifa ipasavyo badala ya kutumikia wanasiasa kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Habari zinazohusiana na hii