• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Hellen Obiri na Daniel Simiu kukosa mkondo wa mwisho wa fainali za mbio za nyika za AK

Hellen Obiri na Daniel Simiu kukosa mkondo wa mwisho wa fainali za mbio za nyika za AK

Na AYUMBA AYODI

HUKU washindi wa mikondo iliyopita wakikosekana, vita vya fainali za mbio za nyika za Shirikisho la Riadha Kenya (AK) sasa ni wazi mkondo wa mwisho utakapoandaliwa mjini Ol Kalou katika Kaunti ya Nyandarua mnamo Januari 2, 2021.

Bingwa wa mbio za nyika duniani Hellen Obiri pamoja na Daniel Simiu, ambaye alinyakua ubingwa wa duru ya ufunguzi mjini Machakos mnamo Novemba 28, wako nchini Uhispania kwa mashindano tofauti.

Obiri anatarajiwa kuwania taji la mbio za kilomita tano kwenye mashindano ya Cursa dels Nassos mjini Barcelona mnamo Desemba 31 naye Simiu atatimka katika mbio za kilomita 10 za San Silverstre mjini Madrid siku hiyo hiyo.

Mshindi wa kitaifa wa mbio za nyika Sheila Chelangat na Charles Yosei, ambao walishinda mkondo wa pili katika eneo la Mosoriot katika kaunti ya Nandi mnamo Desemba 19, pia hawatakuwa Ol Kalou.

Hata hivyo, wakimbiaji 600 wanatarajiwa mjini Ol Kalou. Kwa mujibu wa mwenyekiti wa AK tawi la Nyandarua, Kamau Mfae, idadi kubwa ya washiriki Ol Kalou itatokana na ukaribu wake na mji wa Nyahururu ambao una kambi nyingi za mazoezi.

“Tuna karibu wanariadha 400 wanaofanya mazoezi karibu na mjini Nyahururu. Tunatarajia wanariadha zaidi kutoka viungani mwa Nyahururu. Wanariadha wengi wanatamani sana kurejea mashindanoni baada ya janga la virusi vya corona kuvuruga msimu wao kwa kipindi kikubwa mwaka 2020,” alisema Mfae.

Mfae alifichua kuwa hali ya anga ya joto inayoshuhudiwa katika eneo hilo pamoja na mandhari yako sawa kwa mashindano ya mbio za nyika.

“Tofauti na makala yaliyopita, hali ya anga ya wakati huu hapa ni ya joto. Tumekagua eneo la mashindano na mandhari ni mazuri kwa mbio za nyika,” alisema.

Mkondo wa Ol Kalou uliratibiwa kuandaliwa Januari 9, lakini utafanyika mapema ili kuwapa wanariadha muda mzuri wa kupumzika kabla ya kurejelea mashindano ya kimaeneo na yale ya taasisi yatakayotifua Januari 13.

AK imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na serikali ya kaunti ya Nyandarua kuweka vifaa vya kudumisha usafi katika eneo la mashindano ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. “Wametupatia maji safi, vibanda vya kunawa mikono na pia vyeuzi,” Mfae alisema.

Mbio za Ol Kalou zitafanyika katika bustani ya People’s Park. Zitapisha mbio za nyika za vikosi vya polisi mnamo Januari 15 katika uwanja wa farasi wa Ngong na kisha mbio za nyika za idara ya magereza Januari 16 katika Taasisi ya Mafunzo ya Magereza (PSTC) mjini Ruiru.

Kaunti zote zitaandaa mashindano yao ya mbio za nyika Januari 16 kabla ya majeshi (Januari 29) uwanjani Moi Air Base, huku mashindano ya kimaeneo yakifanyika Januari 30.

Mbio za nyika za kitaifa zitaandaliwa Februari 13 mjini Kisii ambako Kenya itachagua kikosi kitakachoiwakilisha katika Mbio za Nyika za Bara Afrika zitakazofanyika Machi 6 jijini Lome, Togo.

Timu itakayochaguliwa itaingia kambini katika Chuo cha Ualimu cha Kigari katika kaunti ya Embu.

Mashindano ya Bara Afrika yalikuwa yamepangiwa kufanyika Machi 3, 2020. Yaliahirishwa kwa mwezi mmoja kwa sababu ya Uchaguzi Mkuu nchini Togo kabla ya kusukumwa hadi 2021 kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.

Habari hii imetafsiriwa na Geoffrey Anene 

You can share this post!

TAHARIRI: Huu uwe mwaka wa kujirekebisha

Wanasoka saba waliokosea kuondoka Barcelona wakiwemo Neymar...