• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Daraja lililoporomoka Ngoliba lakwamisha shughuli nyingi

Daraja lililoporomoka Ngoliba lakwamisha shughuli nyingi

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa eneo la Ngoliba lililoko Thika Mashariki wameteseka kwa wiki mbili mfululizo baada ya daraja kuu walilokuwa wakitumia kuvunjika ghafla.

Biashara zimesimama huku pia wanafunzi wakipata shida kuvuka ng’ambo nyingine kuelekea Kaunti ya Murang’a.

Wakazi wa eneo hilo waliohojiwa walisema kuwa wamepitia hali ngumu ya kimaisha kwa sababu hadi wakati huu wanalazimika kutumia boti kuvuka hadi upande wa pili.

Hata hivyo Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, katika mahojiano naye alisema wamepata taarifa hiyo na kwa sasa afisi yake inafanya mikakati kuona ya kwamba daraja hilo linarekebishwa haraka iwezekanavyo ili wakazi hao wafanye shughuli zao za kawaida.

“Nilipata ripoti hiyo tayari na ninafanya juhudi kuona ya kwamba daraja la kisasa linajengwa mara moja ili wakazi wa Ngoliba waendeshe shughuli zao kama kawaida,” alisema Bw Wainaina.

Alisema daraja hilo lilikuwa muhimu sana kwa wakazi wa Ngoliba kwa sababu walikuwa wakisafirisha bidhaa zao kutoka upande huo hadi Kaunti ya Murang’a.

Bi Agnes Katulo ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema wamepitia masaibu mengi baada ya daraji hilo kuporomoka.

“Hata wanafunzi wengi hawahudhurii shule kwa sababu ya hali hiyo. Daraja hilo likirekebishwa bila shaka tutarejelea biashara zetu za kawaida,” alisema Bi Kitulo.

Bw David Nzioka ambaye ni mwendeshaji wa boti alisema yeye huvusha watu kwa hadi umbali wa mita 500 katika Mto Chania ambao una viboko hatari.

“Wafanyabiashara wengi huvusha bidhaa zao katika mto huo. Hata wanafunzi wengi huvuka kutoka Ngoliba hadi Iyembeni Secondary upande wa Murang’a,” alisema Bw Nzioka.

Bw Wambua Kiviatu ambaye ni mfanyabiashara eneo la Ngoliba anasema Mto Chania ambako daraja hilo lipo ni hatari kwa usalama kwa sababu ndani kuna viboko wengi.

“Hii ni hasara kubwa sana kwa wazazi kwa sababu kila siku ni lazima walipie Sh20 za kuvushwa na boti hadi upande wa pili,” alisema Bw Kiviatu.

Alisema biashara nyingi zimeharibika kwa sababu ya daraja hilo kuporomoka ghafla.

Alizidi kueleza ya kwamba wakulima wengi ambao husafirisha nyanya, maembe, vitunguu na mboga hupata wakati mgumu kusafirisha bidhaa zao wakati ufaao.

Bi Esther Mutuku ambaye ni mfanyabiashara anasema wanapata hasara kubwa wanapopitisha biadhaa zao kwa kupanda boti.

“Kwa kila mzigo tunalipishwa Sh50 malipo ambayo ni ghali kabisa ikitiliwa maanani kuwa unasafirisha bidhaa nyingi karibu kila mara,” alisema Bi Mutuku.

Bw Stephen Karanja ambaye ni mkazi wa Ngoliba anasema ifikapo majira ya alfajiri na jioni viboko huwa wengi sana katika mto huo wa Chania na kwa hivyo waendeshaji wa boti hizo ni lazima wawe makini wanapovusha watu hadi upande wa pili.

“Iwapo tutarejelea hali yetu ya hapo awali bila shaka kila mmoja wetu atafurahia kwa sababu tutaendelea na shughuli zetu za kawaida,” alisema Bw Karanja.

Bw Jackson Njagi ambaye ni mkazi mwingine wa eneo hilo alisema watu wanaopata shida kubwa ni wahudumu wa bodaboda ambao hulipishwa Sh50 kupitisha pikipiki moja hadi upande wa pili.

“Hata wahudumu wa bodaboda wamepata hasara kubwa sana kwa muda mrefu ambapo daraja hilo likirekebishwa bila shaka biashara zote zitarudi kawaida,” alisema Bw Njagi.

You can share this post!

Wakazi wa Kilifi walalamika kutembea kilomita 10 kutafuta...

Dallas Allstars mabingwa wapya wa Koth Biro