• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Olunga afunga hat-trick akisaidia Al Duhail kukung’uta Al Ahli Doha 6-0

Olunga afunga hat-trick akisaidia Al Duhail kukung’uta Al Ahli Doha 6-0

Na GEOFFREY ANENE

MICHAEL Olunga alifunga ‘hat-trick’ yake ya tano katika soka yake ughaibuni baada ya kuongoza waajiri wake wapya Al Duhail kukung’uta Al Ahli Doha 6-0 kwenye raundi ya 16-bora ya Kombe la Amir mnamo Jumatatu usiku.

Mshambuliaji huyo Mkenya hakuwa amefungia mabingwa hao wa Qatar bao katika mechi zake mbili za kwanza dhidi ya Al Sadd na Qatar SC kwenye Ligi Kuu. Alifuma wavuni penalti safi dhidi ya Al Ahli dakika ya sita kabla ya kuongeza bao la tatu dakika ya 43 na nne dakika ya 69 baada ya Mbrazil Edmilson Junior kufunga la pili dakika ya 22.

Eduardo Pereira Rodrigues (Dudu) aliimarisha uongozi wa Al Duhail hadi 5-0 dakika ya 78 kabla ya Edmilson kuhitimisha dakika ya 90 katika mechi hiyo ambayo beki wa Al Ahli John Benson alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 85.

Olunga alifunga mabao matatu katika mechi moja kwa mara ya kwanza ughaibuni katika klabu ya Girona mnamo Januari 13, 2018. Girona ilibwaga Las Palmas 6-0 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Wakati huo Olunga alikuwa Girona kwa mkopo wa msimu 2017-2018 kutoka Guizhou Zhicheng Hengfeng.

Nchini Japan alikoishi miaka miwili na nusu kutoka Agosti 10, 2018 akichezea Kashiwa Reysol, Olunga alipata ‘hat-trick’ mara tatu. Mabao yake matatu ya kwanza nchini Japan yalikuwa dhidi ya Renofa Yamaguchi katika ushindi wa 4-1 mnamo Agosti 10, 2019 na kufunga mwaka huo katika Ligi ya Daraja ya Pili (J2) na mabao manane katika mchuano mmoja ambao Kashiwa ilizamisha Kyoto Sanga 13-1 Novemba 24, 2019.

Kashiwa ilipandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu (J1) mwaka 2020 baada ya kushinda J2. Alipata ‘hat-trick’ yake ya mwisho kabla ya kuingia Qatar katika mechi kati ya Kashiwa na Vegalta Sendai mnamo Julai 26, 2020. Kashiwa ilipepeta Vegalta 5-1.

Olunga alikamilisha msimu huo juu ya jedwali la wafungaji wa mabao baada ya kutikisa nyavu mara 28, moja zaidi ya mwaka 2019. Alitawazwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora na Kiatu cha Dhahabu wa Ligi Kuu ya Japan mwaka 2020.

Olunga, ambaye klabu yake ya kwanza ughaibuni ilikuwa Djurgardens nchini Uswidi mwaka 2016, alinunuliwa na Al Duhail kutoka Kashiwa kwa ada ya uhamisho inayoaminika kuwa kati ya Sh755 milioni na Sh800 milioni. Kandarasi yake na klabu hiyo inayoshiriki Klabu Bingwa barani Asia na Klabu Bingwa Duniani, ni ya miaka mitatu. Al Duhail ya kocha Sabri Lamouchi itakabana koo na miamba wa Misri na Afrika Al Ahly katika mechi yake ya kwanza kabisa kwenye Klabu Bingwa Duniani hapo Februari 4. Vijana wa Lamouchi ni wenyeji wa dimba hilo. Wakishinda Al Ahly, watamenyana na wafalme wa Bara Ulaya Bayern Munich katika nusu-fainali Februari 7.

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda kwenye ulimi balaa beluwa,...

KCB kufufua uhasama wao na Kabras RFC kwenye raga ya...