• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
AKILIMALI: Mboga ainati za kiasili ndizo tegemeo la riziki

AKILIMALI: Mboga ainati za kiasili ndizo tegemeo la riziki

Na CHRIS ADUNGO

JAMBO ambalo baadhi yao hawalijui ni kwamba kuna njia nyingi mbadala za kujipatia riziki bila ya kutegemea kuajiriwa na mtu katika mazingira rasmi ya afisini.

Benson Kamau, 29, ana mtazamo tofauti kuhusiana na ajira. Yeye hutegemea kilimo cha mboga kujipa riziki ya kila siku, uamuzi ambao umemvunia mafao na nafuu ya kujitegemea kiuchumi.

Mkazi huyu wa kijiji cha Gitaru, eneobunge la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, amejipa ajira ambayo inakidhi mahitaji yake binafsi na ya familia yake change.

Anasema hakufanikiwa kupata elimu ya shule ya upili maanake wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kifedha kumuelimisha zaidi ya kiwango cha shule ya msingi.

Alipohitimisha masomo ya Darasa la Nane mnamo 2004, alianza kazi ya vibarua vya ujenzi wa nyumba, kufanya kazi mashambani mwa watu na wakati mwingine kufanya kazi ya udereva.

Baada ya miaka minne, wazazi walimgawia sehemu ya shamba lao ili ajaribu kilimo. Wazo la kufanya kilimo lilimjia kutokana na kufanikiwa kwa nduguye mkubwa anayejishughulisha pia na kilimo lakini katika eneo tofauti na nyumbani kwao. Kamau aliamua kutumia uzoefu wake, aliokuwa amepata utotoni mwake kutoka kwa wazazi, katika kilimo.

Alianza kwa kupanda aina kadhaa za mboga za kiasili zikiwemo mwangani na mnavu. Anakuza pia sukumawiki, dania, kabichi, karoti na vitunguu maji.

Alichimba mitaro ya maji katika sehemu ya ekari tatu ya ardhi aliyomegewa maanake alijua kwamba mboga zake zingehitaji maji kwa wingi. Zaidi ya hilo, alichimba kisima ili kuhakikisha kuwa katika misimu ya kiangazi, hatakuwa akiathirika kwa kiwango kikubwa. Kwa sasa, Kamau anajivunia kuwa mkulima stadi kwa maana ukulima umemwajiri na huwa unampa

riziki ya kutosha kuyakimu mengi ya mahitaji yake ya kimsingi maishani.

Kazi zinapokuwa nyingi, huwa anaajiri wafanyakazi wa kupanda, kupalilia na kunyunyuzia maji mimea na hata kuvuna. Katika kilimo chake hiki, huwa anatumia mbolea ya wanyama (mboji) na ya kununuliwa madukani ili kuboresha mazao yake. Pia anatumia jenereta maalumu kutoa maji kwenye kisima ili kuhakikisha kwamba

mimea yake inanawiri kwa kupata maji ya kutosha kila wakati.

Kamau hupata mbegu zake zilizopendekezwa na kuidhinishwa na mashirika mbalimbali ya kilimo na huwa zinamsaidia sana kupata mazao mengi na bora.

“Kutokana na mauzo ya mboga hizi, huwa napata angalau Sh20,000 kwa wiki, hivyo basi kila mwezi nina uwezo wa kupata Sh80,000 hivi,” Kamau anaeleza kwa kusisitiza kwamba hiyo ni faida anayosalia nayo baada ya kuondoa gharama zote za kuandaa shamba, kununua pembejeo na kuwalipa wafanyakazi wanaomsaidia shambani.

Yeye huuza mboga za kiasili kwa mafungu ya hadi majani 10 yanayonadiwa kwa kati ya Sh30 na Sh50. Hii ni faida kubwa sana kwake hasa ikizingatiwa kiwango kidogo cha mtaji anaouhitaji ili kuanzisha kilimo chenyewe.

Soko la mboga za Kamau hupatikana katika mitaa ya Kawangware, Gitaru, Kikuyu na Kinoo ambapo huwa anapeleka mboga kuwauzia wafanyabiashara wengi wa rejareja. Hata hivyo, wauzaji wengine huzijia mboga na mazao mengine anayokuza yakiwa bado shambani mwake.

“Ombi langu kwa vijana wenzangu ni kwamba wasichague kazi na kama ingewezakana, nawashauri wengi wajiunge na kilimo maanake kinalipa, na tena ni uti wa mgongo wa taifa,” Kamau ananasihi.

Anasema hana la kujutia tangu aanze kujihusisha na kilimo maanake kimemsaidia kujijengea nyumba ya aushi na ya hadhi na ameweza pia kujenga nyumba za kukodisha ambazo zinamleta mapato mengi zaidi.

You can share this post!

AKILIMALI: Jinsi teknolojia inavyopunguza gharama ya kukuza...

BBI yasababisha mpasuko miongoni mwa madiwani wa Mlima Kenya