Wanaopinga BBI ni wanafiki – Raila

Na SAMMY WAWERU

Kiongozi wa chama cha ODM Bw Raila Odinga amewakosoa wanaopinga mabadiliko ya Katiba, akiwataja kama ‘wanafiki’.

Bw Odinga na ambaye kwa sasa anashirikiana sako kwa bako na Rais Uhuru Kenyatta baada ya wawili hao kuzika tofauti zao za kisiasa kupitia salamu za maridhiano, maarufu kama handisheki, ameendelea kueleza kushangazwa na wakosoaji wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano, BBI inayopendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho.

Kiongozi huyo wa upinzani mnamo Jumanne alisema wanaopinga kupitishwa kwa BBI wakihoji Katiba haipaswi kukarabatiwa, “ni walewale waliopinga ipitishwe 2010”.

Akipigia upatu BBI, alisema wanaopinga Ripoti hiyo ya Maridhiano ni adui wa maendeleo.

“Nimeona kundi fulani likidai linalinda Katiba, linalinda nini? Wanaosema Katiba tuliopitisha ni bora ni walewale walioipinga 2010. Kwa nini useme unailinda sasa, huo ni unafiki wa hali ya juu,” Bw Odinga akasema .

Alitoa matamshi hayo jijini Nairobi kwenye kikao na madiwani, MCA, waliochguliwa kwa tiketi ya ODM, jijini Nairobi.

Akichanganua yaliyomo kwenye BBI, kusaidia kuleta uongozi jumuishi, Odinga alisema marekebisho ya Katiba yatasaidia kuiimarisha.

Baada ya salamu za maridhiano mnamo 2018, makundi ya Kieleweke – linaloegemea upande wa Rais Kenyatta na Odinga, na Tangatanga – upande wa Naibu Rais William Ruto yaliibuka.

Huku Rais Kenyatta na Bw Odinga wakipigia debe kupitishwa kwa BBI, Naibu wa Rais Dkt Ruto ameonekana kupinga kupitishwa kwa mswada huo na pia marekebisho ya Katiba akisema “mjadala unaopaswa kugaragazwa ni unaosaidia kuimarisha maisha ya wananchi.

Habari zinazohusiana na hii

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Kwani kuliendaje?

Raila akausha marafiki