• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Bobi Wine afika mahakamani kupinga ushindi wa Museveni

Bobi Wine afika mahakamani kupinga ushindi wa Museveni

DAILY MONITOR Na SAMMY WAWERU

Mawakili wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine wamewasilisha kesi katika mahakama ya juu zaidi kupinga kuchaguliwa kwa Rais Yoweri Museveni, kufuatia uchaguzi tata uliofanyika mwezi uliopita.

Bw Wine amepinga uhalisia wa matokeo yaliyotangazwa na tume ya kusimamia uchaguzi Uganda, akisema shughuli nzima ya uchaguzi haikuwa ya huru, haki na wazi.

Mwanasiasa huyo ambaye majina yake halisi ni Robert Kyagulanyi, aliibuka wa pili katika uchaguzi huo wa mnamo Januari 14, nyuma ya Rais Museveni.

Zoezi hilo limetajwa kuwa mbaya zaidi katika historia ya Uganda, kufuatia ghasia zilizozuka na kusababisha maafa na umwagikaji wa damu.

Bw Medard Sseggona, ambaye ni mmoja wa mawakili wa Wine alisema uchaguzi wowote Rais Museveni hushiriki hauwezi ukawa wa amani, wala wa huru na haki.

“Tunataka matokeo ya uchaguzi huo yafutiliwe mbali. Hatutaki Museveni ashiriki uchaguzi mwingine siku za usoni,” Bw Sseggona akaambia wanahabari nje ya majengo ya mahakama ya juu zaidi Uganda, Kampala.

Rais Museveni, 76, na ambaye ametawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 34, tangu 1986, katika uchaguzi wa 2021 aliibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 59 ya kura zilizopigwa kutawala, awamu ya sita.

Alitetea kuhifadhi kiti chake kwa tiketi ya chama cha NRM. Bw Wine, 38, alipata asilimia 35 ya kura, akitaja zoezi hilo kama lililokumbwa na utapeli na wizi wa kura.

Chini ya Katiba ya Uganda, Wine ana siku 15 pekee kukata rufaa tangu tume ya uchaguzi, UEC, ilipotangaza rasmi matokeo. Mahakama ya juu zaidi nchini humo ina chini ya siku 45 pekee kusikiliza kesi na kutoa maamumizi.

Kesi za wagombea urais waliobwagwa Uganda miaka ya awali, wanaopinga matokeo hazijawahi kufua dafu. Wakili Sseggona alisema wanajeshi walikuwa wakiingia kwenye vituo vya kupigia kura na kujaza masunduku kwa kura za kumchagua Museveni.

Wakili huyo pia alidai sajili za wapiga kura katika baadhi ya vituo zilikuwa zimehitilafiwa. “Museveni hawezi kuachiliwa kuiba kura kisha awe huru,” Sseggona akasema.

Rais Museveni kwa upande wake amesema uchaguzi wa 2021 ulikuwa wa huru, haki na uwazi zaidi ukilinganishwa na chaguzi za awali na katika historia ya Uganda.

Kabla, wakati na baada ya zoezi hilo, vurugu na ghasia zilishuhudiwa. Novemba 2020, zaidi ya wafuasi 54 wa Bobi Wine waliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa usalama, wakati wakiandamana kushinikiza aachiliwe huru.

Kiongozi huyo wa chama cha NUP amekuwa akikamatwa mara kwa mara na kuhangaishwa na serikali ya Museveni.

Baada ya uchaguzi, makazi yake yalizingirwa na maafisa wa kijeshi Uganda, makama nchini humo ikiwaamuru waondoke mara moja.

Kuanzia Jumatatu, wanajeshi wamekuwa wakionekana kushika doria katika barabara mbalimbali Uganda.

Rais Museveni anaendelea kukosolewa kutokana na uongozi wake unaotajwa kuwa wa kimabavu, kukiuka demokrasia ya wapinzani wake.

You can share this post!

Wanaopinga BBI ni wanafiki – Raila

Tanzania yakana mpango wa kufungia raia makwao kuepuka...