• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Muuguzi asimulia alivyolazimishwa kupashwa tohara akiwa na miaka 6

Muuguzi asimulia alivyolazimishwa kupashwa tohara akiwa na miaka 6

WAWERU WAIRIMU Na SAMMY WAWERU

Bi Rosaline Guyo Gollo alikuwa na umri wa miaka sita pekee alipolazimishwa kupashwa tohara (FGM). Taswira ya mazito na machungu aliyopitia chini ya aliyempasha tohara chini ya mti katika kijiji cha Lakole, Merti, Kaunti ya Isiolo ingali mawazoni mwake kufikia sasa.

FGM ni ukataji wa kiungo kwenye sehemu nyeti ya mwanamke. Anakumbuka barabara kana kwamba ilikuwa jana tu, siku ya tukio jamaa zake walimtoa shuleni pamoja na dada yake mwenye umri wa miaka minane, wakawapeleka kwa dada ya nyanya yao, ambaye waligundua ndiye alipaswa kutekeleza tendo hilo haramu.

Kwa nyanya huyo, anakumbuka kulikuwa na makumi ya wasichana wadogo na ambao walizungukwa na wanawake wakongwe. Nduru zilikuwa zikiskika kutoka kwenye mojawapo ya chumba.

“Dadangu alipelekwa kwa nguvu katika chumba hicho, na dakika chache baadaye nikaskia akipiga kamsa nikajua mambo si shwari,” Gollo aelezea.

Hofu ilimgubika na akajaribu kutoroka baada ya kuona hali aliyopitia dada yake huku akipelekwa katika chumba kingine, kilichokuwa pembezoni.

Jitihada zake kutoweka hata hivyo hazikuzaa matunda, kwani vijana kadha akiwemo kaka yake walimkamata na kumrejesha.

Alipelekwa katika chumba kilichogeuzwa ukumbi wa shughuli hiyo haramu, FGM.

“Baadhi ya wanawake walinifunga kwa kamba, nyanya yule akiniagiza nitawanye miguu. Nusra nikate roho kutokana na uchungu niliohisi na uliosheheni mwili mzima, nikikatwa kwa wembe,” anasimulia.

Kuvuja damu na ukaguzi zaidi

Kilele cha tendo alilopitishw, kiliishia kufuja damu kwa muda wa mwezi mmoja, miaka sita iliyofuata akawa akipitia matatizo kiafya.

Shangazi yake alipogundua tohara aliyopashwa haikufanywa ilivyofaa, alipendekeza akaguliwe zaidi.

“Tendo nililopitia mara ya kwanza lilikuwa bichi sana mawazoni. Walinipeleka kwa mkunga, na licha ya kujaribu kuhepa sikufanikiwa,” Gollo anasema.

Baada ya ukaguzi mwingine, ‘mkato’, alipoteza fahamu, akakimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Merti ambapo alifanyiwa matibabu.

Anasema asingeweza kuenda haja ndogo, kwa sababu ya madhara ya tohara.

“Nilishangaa kujipata nimelazwa hospitalini. Nilihisi uchungu usiomithilika, nikawa dhaifu, kilichosalia maishani mwangu kikawa kuomba nife,” anaelezea mama huyo.

Miaka kadha baadaye, Bi Gollo aligundua asingeweza kujifungua mtoto kwa hali na njia ya kawaida ya uzazi kwa sababu ya athari za tohara kwenye sehemu nyeti yake.

Tembe chungu kumeza, ikawa atajifungua kwa njia ya upasuaji (maarufu kama CS), hatua ambayo ni hatari.

Ni mama wa wasichana wanne, wote akijifungua kwa njia ya upasuaji. Aidha, alipoteza mtoto wake wa kipekee wa kiume wakati akijifungua, tukio ambalo lilisababisha utumbo wake wa uzazi kufungwa kabisa, hii ikiwa na maana kuwa hawezi kupata watoto wengine maishani.

Katika jamii anayotoka, inaaminika mwanamke aliyepitia FGM ada ya mahari kwa wazazi wake ni ya juu, hivyo basi kuiletea fahari familia.

Kwa wale ambao hawajapashwa tohara, wanachukuliwa kama ‘laana na wanawake wachafu’ katika jamii.

Ingawa sababu za FGM zinatofautiana katika jamii mbalimbali ambazo hutekeleza tendo hilo haramu, nyingi hupasha wasichana wao ili wasishiriki ngono kabla ya kuoleka.

Kulingana na takwimu za Unicef 2020, zaidi ya wasichana milioni nne nchini Kenya wamepashwa tohara.

Hata hivyo, Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2019 alisema idadi ya wasichana waliopitia FGM nchini ni milioni 9.3.

Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 wamepashwa tohara katika mataifa 30 Barani Afrika, Bara la Kati na Asia ambapo wengi hupitia FGM pindi wanapozaliwa hadi wanapofikisha umri wa miaka 15.

Bi Rosaline Gollo, muuguzi wa Isiolo, asambaza bidhaa kwa wasichana eneo la Merti, Kaunti ya Isiolo. PICHA/ WAWERU WAIRIMU

FGM huwaweka wasichana katika hatari ya kufuja damu, matatizo ya haja ndogo na kuathiri mpangilio wa siku za hedhi, ikiwa ni pamoja na mahangaiko wakati wa uzazi na hatari ya watoto kufariki wakati wa kujifungua.

Wengi wa waliopitishwa tohara huogopa kujitokeza, kwa hofu ya kupitia unyanyapaa katika jamii.

Bi Gollo ameonyesha ukakamavu na ujasiri wa hali ya juu kueleza mahangaiko aliyopitia, kwenye masimulizi yake, akieleza bayana asingetaka kuona msichana au wasichana wakipashwa tohara.

Imemchukua kipindi cha miaka 31 kwa mwanaharakati huyo wa vita dhidi ya FGM, kufichua aliyopitia, hasa baada ya kuzindua Shirika la Kijamii – CBO maarufu kama Waso Hope, lenye shabaha kufanya hamasisho la athari za FGM.

Wasichana wanaopashwa tohara kuozwa mapema

Mbali na Waso Hope kujituma katika vita dhidi ya FGM, shirika hilo pia linaendelez kampeni kuangazia vita vya kijinsia, ndoa za mapema, na kuripoti visa kwa idara husika ili hatua zichukuliwe.

Kwa ushirkiano na wadau husika, shirika la mama huyo pia hufanya hamasa ya masuala ya afya, kutoa huduma za ukaguzi wa Sratani ya sehemu nyeti za wanawake, kusambaza sodo kwa wasichana wa shule na pia utoaji ushauri haja ya kukumbatia mbinu kudhibiti uzazi – matumizi ya dawa za uzazi.

“Nilihisi machungu, ila nikaamua kusahau niliyopitia ili niwe na amani,” Bi Gollo akasema wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Kwa mujibu wa ripoti ya KDHS ya 2014, visa vya FGM Kenya vimesimamia asilimia 21, na vinakadiriwa kutekelezwa na zaidi ya asilimia 50 ya baadhi ya jamii, ile ya Wasomalia ikiongoza kwa asilimia 94, inafuatwa kwa karibu na jamii ya Samburu 86, na Maasai 78.

Bi Gollo huendesha kampeni yake katika masoko, makazi ya watu na maeneo mbalimbali ya umma katika Kaunti ya Isiolo, ambapo visa vya tohara vinaendelezwa, hata ingawa anathibitisha baadhi wameasi tendo hilo potovu.

Mama huyo ambaye pia ni muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Isiolo, anasema iwapo angekuwa na uamuzi asingepitishwa tohara, huku akiapa katu wasichana wake hawatapashwa.

Kupitia huduma zake kwa jamii, Bi Gollo pia hutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa na kuwaelekeza katika vituo vya kuwanusuru, ili kuponya nafsi zao.

Mwanaharakati huyo pia hutoa huduma zake kupitia mitandao ya kijamii. Oparesheni yake imeweza kuleta pamoja wanawake wapatao 15 kote nchini, na ambao humsaidia kuendesha kampeni.

“Nimeweza kuhamasisha wavulana 1, 000 na wasichana 2, 500 eneo la Merti, ambapo tumeunda makundi kueneza athari za FGM. Wasichana hao hupata sodo na wavulana vitabu,” Gollo anadokeza.

Kupitia jitihada zake, anasema wapashaji tohara 10 wameasi shughuli hiyo haramu, ila anaihimiza serikali kuwatafutia njia mbadala kujiendeleza kimaisha.

Kipindi cha Covid-19

Mama huyo anasema katika kipindi hiki cha Covid-19, kumekuwa na ongezeko la idadi ya wasichana wanaopashwa tohara, mimba za mapema na baadhi kuozwa, hasa wakati ambapo sheria za kusafiri ili kuzuia msambao wa corona zilikuwa zinatekelezwa.

Kufikia Desemba 2020, Gollo anafichua alikuwa ameokoa wasichana saba, akiwemo wa darasa la nane mwenye umri wa miaka 14 ambaye alibakwa eneo la Gafarsa, na wengine wawili waliolazimishwa kupashwa tohara Kinna.

Huku dunia ikiadhimisha siku ya kimataifa dhidi ya FGM, Gollo anafanya kampeni na wadau husika, lengo lake likiwa kusaidia Rais Uhuru Kenyatta kuafikia kuangamiza tendo hilo haramu kufikia 2022, hasa katika kaunti 22 ambazo zimetajwa kuwa hatari.

Bi Mumina Jirmo, mwathiriwa wa FGM anahimiza mama huyo kutokata tamaa katika maazimio yake. Bi Gollo, 45, ameweza kuleta pamoja wahubiri kadha anaotaja wamekuwa na mchango mkuu kusaidia kuangazia FGM Isiolo.

Mwanaharakati huyo anahimiza waliopitia tendo hilo kujitokeza na kuwapa motisha wengine, katika mdahalao mzima kuangazia FGM.

Ukosefu wa vituo kuokoa waathiriwa, wakati sheria ikichukua mkondo wake, ni baadhi ya changamoto ambazo Bi Gollo anapitia.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, matibabu ya matatizo yanayotokana na athari za FGM hugharimu zaidi ya Sh140 bilioni kwa mwaka katika mataifa 27 yaliyotajwa kuathirika pakubwa.

You can share this post!

Akamatwa baada ya kuua mkewe na watoto wake wawili

Nitamwambia Uhuru akutimue, Atwoli amtishia Kagwe