• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AKILIMALI: Mwanafunzi wa JKUAT avuna hela kwa kukuza matundadamu

AKILIMALI: Mwanafunzi wa JKUAT avuna hela kwa kukuza matundadamu

Na SAMMY WAWERU

ZIARA aliyofanya Charity Kigera kwa mkulima mmoja wa matundadamu Nyandarua mapema 2019 ilichochea ari yake kuingilia kilimo cha matunda.

Msichana huyu ambaye yuko mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), anakosomea kozi ya Masuala ya Savei, anasema alikaribishwa na miti ya matundadamu maarufu kama tree tomato pia tamarillo iliyozaa matunda yaliyonawiri.

“Alinichumia tunda na nilipolikumbatia lilijaa kwenye kiganja cha mkono,” anasema Charity, 25, akielezea kwamba mkulima huyo alikuwa na miti mitano pekee.

Anafafanua, ilizaa matunda kiasi kwamba akihesabu kila tawi lilikuwa na matundadamu yasiyopungua 14. Taswira hiyo ilimshawishi, na huo ukawa mwanzo wa safari yake katika kilimo.

Charity anasema hakulila. Alienda nalo nyumbani akiwa na wazo, wazo atakavyokuwa mkulima wa matundadamu.

Ikizingatiwa kuwa ni mwanafunzi, alizungumza na babake ambaye pia ni mkulima ingawa wa viazi na mahindi, akamuarifu mipango yake chipuka. Hakusita kumpa kipande cha ardhi atimize matamanio yake.

“Nililikama, nikatoa mbegu zake, nikaziosha na kuzikausha kwenye kivuli kwa muda wa wiki moja na nusu hivi,” anaelezea, akisema utafiti aliofanya mitandaoni kupitia makala ya ukuzaji wa matundadamu ulimshauri asizikaushe kwenye jua.

Anasema miale ya jua huharibu machipukizi ya mbegu, kauli yake ikipigwa jeki na David Nderitu mkulima hodari wa matundadamu Nyeri.

“Miche ya matundadamu inatokana na mbegu za matunda makubwa yaliyokomaa, yakanawiri na ambayo mti mama umestawi na wenye afya,” Nderitu anasema, akiongeza kuwa gharama ya kununua miche inaweza kuondolewa kwa kujikuzia.

Tundadamu linakadiriwa kuwa na kati ya mbegu 200 – 400, Charity Kigera akieleza kwamba ilimchukua kipindi cha muda wa miezi mitano kuandaa miche.

“Uamuzi wa kuingilia kilimo ulienda sambamba na kipindi ambacho nilikuwa nimetumwa kufanya mazoezi ya kozi ninayosomea,” anadokeza mkulima huyu mchanga.

Charity anasema alikuwa ameandaa jumla ya miche 270, ila alipanda 200 kwenye robo ekari, iliyosalia akawapa majirani. Kwa kuzingatia taratibu faafu kitaalamu, ekari moja inaweza kusitiri karibu mitundadamu 1, 000.

Amekumbatia mfumo wa kilimohai, na anaiambia Akilimali kwamba alitumia mbolea ya mifugo, hususan mbuzi katika shughuli za upanzi.

Badala ya kutumia fatalaiza kunawirisha mazao, Charity anasema kwenye mashina ya mitundadamu aliweka mbolea ya mbuzi ‘iliyoiva’ vizuri.

Magonjwa yanayoathiri tamarillo ni sawa na ya matunda mengine, ila kwa mkulima huyu anasema hakushuhudia ugonjwa wowote.

“Wadudu walioonekana japo niliwakabili kwa dawa ni vidukari,” anasema.

Matunzo mengine aliyofanya ni palizi dhidi ya kwekwe, kupogoa matawi ili kuondoa ushindani, na kunyunyizia maji hasa mitundadamu ikiwa michanga na ilipoanza kuchana maua na kutunda.

Charity Kigera mwanafunzi wa JKUAT ambaye anakuza matundadamu. Picha/ Sammy Waweru

“Kwetu tuna kisima chenye urefu wa futi 100, ambacho hutumia nguvu za umeme kupampu maji, hivyo basi mahangaiko ya maji hayapo,” anaelezea.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanasema ufanisi katika uzalishaji wa matunda unategemea kuwepo kwa maji ya kutosha.

“Kilimo chochote kile cha matunda kinafanikishwa na uwepo wa maji ya kutosha,” anasisitiza mtaalamu Daniel Mwenda, akihimiza wakulima kukumbatia mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji.

Kulingana na Charity, changamoto kuu iliyomkumba ni matawi kuanguka, kwa kile anataja kama “matundadamu kuzaa ajabu”. Kibarua kikawa kuyasitiri kwa miti.

Kijiji cha Bahati, Gathanje, Kaunti ya Nyandarua, ni tajika katika ukuzaji wa viazi na mahindi, ila katika shamba la msichana huyu, taswira ni tofauti kabisa. Ni bustani ambalo linavutia kutokana na alivyolirembesha kwa matundadamu.

Alianza kufanya mavuno Novemba 2020, na kutokana na yalivyonawiri hofu yake ilikuwa moja tu; “Nitapata wanunuzi ilhali yamezaa kiasi cha kuangusha matawi?”

Ni wasiwasi uliomchochea kuyapiga picha na kuzipakia kwenye makundi yanayotoa huduma za kilimo mitandaoni.

Anasimulia kwamba majibu aliyopata, ya oda, yamemuacha kujutia ni heri angeyakuza kwenye ekari moja au hata zaidi.

“Wengi walikuwa wanunuzi wa kijumla wanaoagiza kilo zisizopungua 200, na kilichonishtua zaidi ni huyu mkulima aliyeniuliza ikiwa mazao niliyonayo yanaweza kujaa gari aina ya Probox,” anafafanua.

Ni gapu ya uhaba wa matundadamu aliyotambua Charity, kuanzia mwaka huu wa 2021 akipanga kuyalima kwenye ekari moja. Kutokana na oda alizopata, anakiri kiwango cha uzalishaji wa matundadamu Kenya ni cha chini sana, kikilinganishwa na walaji.

Ingawa yaliyoiva shambani yameisha, anasema kufikia sasa ameuza zaidi ya kilo 200, kila kilo ikinunuliwa Sh70.

“Cha kustaajabisha, miti inaendelea kuchana maua na kutunda,” anaeleza. Akifanya hesabu, anasema gharama aliyotumia kufikia sasa haizidi Sh5,000.

Huku akisubiri kufuzu kozi anayosomea JKUAT, licha ya mkurupuko wa janga la Covid-19 mwaka uliopita wa 2020 kuathiri kalenda ya masomo nchini, Charity anasema hatua aliyochukua kuingilia kilimo ni maandalizi ya jukwaa kujiajiri kupitia zaraa.

“Ndoto zangu zimekuwa kufanya kilimo cha matunda kama gange ya ziada, hata nikipata ajira nitakapohitimu chuoni. Nafasi za kazi za ofisi Kenya ni finyu mno, maelfu ya vijana waliofuzu kwa taaluma mbalimbali wakiendelea kuhangaika kwa kukosa ajira,” anasema, akishauri vijana kuthamini kilimo.

Anafichua, kwa sasa amejituma kufanya utafiti namna ya kuongeza matundadamu thamani, kutengeneza bidhaa zitokanazo nayo.

You can share this post!

Wezi wavamia makazi ya meya wa zamani wa Thika

West Brom wakaba koo Man-United na kudidimiza matumaini yao...