• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Wezi wavamia makazi ya meya wa zamani wa Thika

Wezi wavamia makazi ya meya wa zamani wa Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WEZI walitekeleza uvamizi wa kimabavu katika makazi ya meya wa zamani wa Thika Bw David Njehia na kuiba mbuzi wapatao 40, kabla ya kumkata shingo mlinzi mmoja na kumuua.

Mbuzi watatu walipatikana nje ya lango wakiwa wamekatwakatwa vipande.

Wezi hao waliovamia kijiji cha Kahonoki, Ndula, Thika Mashariki, walikuwa na mapanga, rungu na shoka na walitekeleza unyama huo saa tisa alfajiri Jumamosi.

Kulingana na mkazi mmoja wa kijiji hicho, Bw John Mwaura, wezi hao walivunja lango kuu la boma hilo na kuingia ambapo mlinzi aliyekuwa langoni alikatwa kichwa na kufariki papo hapo.

“Tulisikia mayowe na tulipotoka nje tulipata mlinzi amelala chini akiwa anavuja damu kwa wingi,” alisema mkazi hiyo.

Mfanyakazi mwingine aliyejaribu kutoka nje usiku alishambuliwa na kujeruhiwa kichwa vibaya huku akiachwa hali mahututi.

Bw Njehia ambaye boma lake lilivamiwa alisema yeye hakuwepo, lakini aliarifiwa baadaye.

“Nilipofahamishwa kuhusu tukio hilo nilipiga ripoti kwa polisi mara moja ambapo walifika eneo la tukio,” alisema Bw Njehia.

Alisema amesikitishwa na tukio hilo ambapo hali ya usalama imezorota katika kijiji hicho.

“Ningetaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kujua kiini cha wezi hao kuvamia boma langu hasa nyakati kama hizo za alfajiri. Hata nahofia maisha yangu kwani wangalinipata pengine wangaliniangamiza,” alisema kiongozi huyo.

Alisema polisi wameanza uchunguzi huku wakimhakikishia kuwa watafanya juhudi kuona wahalifu hao wananaswa.

Wakazi wa kijij hicho wanaitaka serikali kuingilia kati ili kuona ya kwamba inajenga kituo cha polisi katika kijiji hicho.

Tayari tukio hilo limeacha wakazi hao na hofu tele huku wakisema wezi hao wanastahili kusakwa na kuchukuliwa hatua ya kisheria.

Eneo hilo liko takribani kilomita 25 hivi kutoka mji wa Thika.

  • Tags

You can share this post!

Kibarua cha Gor Mahia kukabiliana na mikosi ya ugenini soka...

AKILIMALI: Mwanafunzi wa JKUAT avuna hela kwa kukuza...