• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
BBI yaunganisha vigogo wa Mulembe

BBI yaunganisha vigogo wa Mulembe

Na SHABAN MAKOKHA

MIITO ya kutaka viongozi wa eneo la Magharibi kuungana ilitawala mkutano wa mashauriano kuhusu mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) uliofanyika mjini Kakamega.

Mkutano huo uliwaunganisha viongozi ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa mahasimu wa kisiasa.Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula hawajakuwa wakitangamana na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.

Viongozi hao watatu wametangaza azma yao ya kutaka kuwania urais 2022.Katika mkutano huo wa Jumamosi, Bw Mudavadi, Seneta Wetang’ula na Gavana Oparanya waliketi pamoja huku wakifuatilia kwa karibu maoni yaliyokuwa yakitolewa na madiwani kutoka eneo la Magharibi kuhusiana na mswada wa BBI.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli, waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, magavana Sospeter Ojaamong (Busia), Wycliffe Wangamati (Bungoma), Wilbur Ottichilo (Vihiga), na wabunge Chris Wamalwa (Kiminini) na Alfred Agoi (Sabatia).

Seneta wa Bungoma Wetang’ula alisema kuwa viongozi wote wa Magharibi wameungana na wanaunga mkono BBI. “Hiyo ndiyo maana nimeketi hapa kama ishara kwamba ninatembea na Wakenya wengine pamoja. Lakini umoja huu unafaa kuendelea hata baada ya BBI ili miradi ya maendeleo yaweze kufikia wakazi wa eneo hili,” akasema Bw Wetang’ula.

Alisema kuwa viongozi wa Magharibi wanapotofautiana na kutupiana cheche za maneno, wakazi wanakosa kunufaika na maendeleo.

“Kwa sababu Rais Kenyatta anastaafu mwaka ujao, ni jukumu letu kuungana na kutumia wingi wetu kuchukua hatamu za uongozi wa taifa hili,” akasema Bw Wetang’ula.

Alionya kuwa jamii ya Waluhya hata ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, haitaweza kutwaa uongozi wa nchi iwapo itaendelea kugawanyika.

Kauli hiyo ya kiongozi wa Ford Kenya iliunga mkono na Bw Atwoli na Bw Mudavadi. Katibu Mkuu wa Cotu alisema kuwa yeye ndiye mwasisi wa BBI.“Mnamo Mei 1, 2017, wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi, nilipendekeza kuwa kulikuwa na haja ya kuchunguza upya Katiba yetu kuhakikisha kuwa hakutakuwa na mapigano kila baada ya uchaguzi mkuu. Ninafurahi kuona kwamba pendekezo hilo lilikumbatiwa na Rais Uhuru Kenyatta,” akasema.

Bw Atwoli alisema kuwa eneo la Magharibi linaweza kutoa mtu atakayekuwa rais wa tano wa Kenya endapo wataungana na kuzungumza kwa sauti moja.

Bw Mudavadi na Bw Oparanya wamekuwa wakipigania uongozi wa kisiasa wa eneo la Magharibi licha ya kiongozi wa ANC kutawazwa kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya na Bw Atwoli mnamo Novemba 30, 2016 katika uwanja wa Bukhungu.

You can share this post!

Seneta wa Garissa Yusuf Haji afariki

Maangi na Osoro wakamatwa katika mazishi ya Nyachae