• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Rashford awabeba Manchester United dhidi ya Newcastle katika EPL

Rashford awabeba Manchester United dhidi ya Newcastle katika EPL

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Marcus Rashford alichangia pakubwa ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na waajiri wake Manchester United kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Newcastle United mnamo Februari 21, 2021 ugani Old Trafford.

Nyota huyo raia wa Uingereza alifungia Man-United bao la kwanza katika dakika ya 30 na kuchangia la pili lililofumwa wavuni na Daniel James kunako dakika ya 57 baada ya Allan Saint-Maximin kuwarejesha Newcastle mchezoni katika dakika ya 36. Goli la Rashford lilikuwa lake la 18 kufikia sasa msimu huu.

Saint-Maximin alikuwa akichezea Newcastle kwa mara ya kwanza baada ya ugonjwa wa Covid-19 kumweka nje kwa zaidi ya kipindi cha miezi miwili iliyopita. Bao lake lilitokana na utepetevu wa beki na nahodha wa Man-United, Harry Maguire.

Rashford alichangia tena penalti iliyompa kiungo Bruno Fernandes kufungia Man-United goli la tatu katika dakika ya 75 baada ya chipukizi Joe Willock anayechezea Newcastle kwa mkopo kutoka Arsenal kumkabili Rashford vibaya ndani ya kijisanduku. Bao hilo la Fernandes ambaye ni raia wa Ureno, lilikuwa lake la 22 kufikia sasa msimu huu.

Kichapo ambacho masogora wa Newcastle wanaonolewa na kocha Steve Bruce walipokezwa kilikuwa chao cha nane kutokana na mechi 10 zilizopita za EPL. Matokeo hayo yaliwasaza katika nafasi ya 17 kwa pointi 25, tatu pekee mbele ya Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion na Sheffield United, wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Kwa upande wa Man-United wanaotiwa makali na kocha Ole Gunnar Solskjaer, ushindi huo ulikuwa wao wa pili kutokana na mechi sita zilizopita za EPL. Walijibwaga ugani wakilenga kujinyanyua baada ya West Brom kuwalazimishia sare ya 1-1 katika mechi yao iliyopita.

Licha ya ushindi, pengo la pointi 10 bado linatamalaki kati ya Man-United na viongozi wa jedwali Manchester City waliowapiga Arsenal 1-0 katika mchuano mwingine wa EPL mnamo Jumapili usiku. Man-United kwa sasa wanajivunia alama 49 sawa na nambari tatu Leicester.

Man-United kwa sasa wamefunga jumla ya mabao 53 kutokana na mechi 25 za hadi kufikia sasa msimu huu, hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi ya magoli kufikia hatua hiyo kwenye kampeni za EPL tangu msimu wa 2012-13 ambapo walikuwa wamefunga magoli 60 kabla ya hatimaye kutawazwa wafalme wa ligi.

Kwa upande wao, Newcastle wamepoteza sasa mechi zote 21 zilizopita za ugenini dhidi ya vikosi vinavyoshikilia nafasi tatu za kwanza jedwalini tangu Februari 2012.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuonana na Real Sociedad katika marudiano ya hatua ya 32-bora ya Europa League mnamo Februari 25. Watajibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakijivunia ushindi mnono wa 4-0 katika mkondo wa kwanza. Baada ya hapo, watakuwa wenyeji wa Chelsea katika mchuano wa EPL utakaowakutanisha ugani Stamford Bridge mnamo Februari 28.

Newcastle watakuwa wenyeji wa Wolves ugani St James’ Park kwa minajili ya gozi la EPL mnamo Februari 27, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

ICC huenda ifute dhamana kwa wakili Gicheru

Monaco yaduwaza PSG kwa kuipiga 2-0 kwenye Ligue 1