Mama amlaani mwanawe kortini

Na RICHARD MUNGUTI

MAMA wa umri wa makamo alishangaza wengi alipomlaani mwanawe mbele ya mahakama.

Bi Phelister Akinyi alifika mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Makadara na kumlaani mwanawe Fredrick Ochieng aliyetisha kumuua siku kikuu ya wapendanao almaarufu Valentine.

Mama huyu aliyekuwa amejawa na hamaki alieleza mahakama kuwa mwanawe huyo aliyemkodishia nyumba amekuwa mtoto “msumbufu na mkorofi.”

Mshtakiwa alielezwa wazi wazi kortini na mama yake “ mateso unayonisumbua na kutisha kuniua hautaona amani duniani..mimi ni mama yako niliyekuzaa. Sio wewe ulinilea ni mimi. Kila mara unakuja kunibishia mlango na kunikeleji mbele ya majirani.Hutaki kusoma . Hutaki kufanyakazi. Unataka kustarehe tu na pesa zangu kisha watisha kuniangamiza.”

Akinyi alifika kortini na kuomba hakimu amsukume mwanawe gerezani kwa sababu amekuwa akitisha kumuua.

“Nataka nikueleze papa hapa mbele ya kila mtu na hakimu..ukiniua utakuwa ukinipata kila mahali,” Akinyi aliyekuwa mwingi wa hasira alimweleza mwanawe mbele ya umati wa watu kortini waliomtazama kwa mshangao.

Mama huyo aliendelea , “ Ukienda chumba cha mazugumzo utanikuta uko. Ukienda chumba cha malazi (bedrumu) utanikuta uko, ukienda kwa choo utanikuta uko, ukienda bafu utanikuta uko.”

Fredrick Ochieng akiwa kizimbani mahakama ya Makadara. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Mama huyo aliomba msaada wa mahakama akisema “ mimi nimefika mwisho. Naomba hii mahakama inisaidie. Huyu mtoto ni mtukutu. Kila ninapoenda Benki yeye unifuata uko kuangalia nitatoa pesa gapi kwa akaunti yangu.”

Alisema punde tu anapowasili kwa nyumba mwanawe huyo humwandama na kuanza kumndadizi kile alichotenda na pesa alizotoa kwa akaunti.”

“Nataka nikueleze kuwa , pesa ni zangu. Utaenda kufanya kazi upate zako uwe ukitumia jinsi upendavyo,” Akinyi alimweleza mwanawe huku akichemka kwa hasira.

Mama huyo alifichua kwamba ndiye amemkodishia nyumba anakoishi na mkewe.

“Huyu kijana hafanyi kazi. Ni mimi ninaye mlipia nyumba tangu awache kazi katika kituo kimoja cha habari nchini. Hata juzi nimenunulia mkewe chakula ya Sh4,000 na huyu anakuja kwangu Greenfield kunikemea,”alisema Akinyi.

Alisema mwanawe huyo amekuwa akimtisha na kusema “ hawezi ogopa polisi labda ashikwe na maafisa wa kikosi cha polisi cha kupambana na ghasia almaarufu GSU ama kikosi cha Jeshi la Nchi Kavu.”

Mama huyo aliomba korti isithubutu kumwachilia mwanawe kwa vile atatekeleza vitisho vyake.

“Mimi nimeililia mahakama. Ni jukumu lako hakimu unitunze na kunilinda. Naomba sheria iwe ngao yangu na mhifadhi wangu.”

Fredrick alikanusha shtaka la kumtishia mama yake maisha na kuhatarisha amani.

Mahakama iliamuru azuiliwe gerezani huku mahojiano zaidi yakifanywa na idara ya urekebishaji tabia kumuhusu mshtakiwa na ripoti kuwasilishwa kortini.