• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 AM
Raia wa TZ akana kuuza vifaa feki vya kupima Ukimwi Kenya

Raia wa TZ akana kuuza vifaa feki vya kupima Ukimwi Kenya

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Tanzania anayefanya biashara nchini Kenya Jumatatu alishtakiwa kwa kuuza vifaa feki vya kupima ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Bw Issa Uledi Kawaya alifikishwa mbele ya hakimu mkuu Bi Martha Mutuku na kusomewa shtaka.

Alikanusha kuwa kati ya Septemba 24 na Desemba 30 2018 akishirikiana na wafanyabiashara wengine aliingiza humu nchini pakiti 400 za vifaa ghushi vya kupima maradhi ya ukimwi.

Kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda alimweleza hakimu kuwa Bw Kawaya aliingiza nchini vifaa hivyo feki akidai ni zile za muundo wa Uni-Gold.

Vifaa hivyo , Bw Gikunda , alisema vilikuwa na thamani ya Sh800,000.

Hakimu alifahamishwa Bw Kawaya aliziingiza vifaa hivi bila idhini ya kampuni ya Trinity Biotech iliyosajiliwa kuuza vifaa vya Uni-Gold.

Ni Trinity Biotech inayokubaliwa kuweka chapa cha Uni-Gold kwenye bidhaa za kupima ukimwi.

“Bw Kawaya umeshtakiwa kuuza vifaa feki vinavyofanana na vile vinavyouzwa na kusambazwa na kampuni ya Trinity-Biotech,” Bw Gikunda alimweleza mshtakiwa.

“Sio ukweli Mheshimiwa,”Bw Kawaya alimjibu hakimu.

Mshtakiwa huyo pia alielezewa kuwa alikaidi sheria zinazothibiti uuzaji wa bidhaa halisi Sehemu ya 35(a) iliyotungwa na kuchapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali nambari 13 mwaka wa 2008.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana na kumweleza hakimu , “ Mimi ni raia wa Tanzania na nimeishi humu nchini miaka 21. Nimeoa Mkenya na kamwe sitatoroka niache familia.”

Bw Kawaya aliendelea kusema kuwa amekuwa akifanya biashara humu nchini.

Mahakama ilifahamishwa wiki mbili zilizopita wafanyabiashara wengine walishtakiwa na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu kila mmoja.

Hakimu alimwachilia Bw Kawaya kwa dhamana ya Sh300,000 pesa tasilimu na kuamuru kesi itajwe Machi 8,2021 kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

Raia wa Burundi na Mali wamlaghai Mlebanon Sh7m

Mama amlaani mwanawe kortini